William Ruto amekana mashtaka yote yanayomkabili kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama hiyo, Fatou
Bensouda anayesimamia kesi hiyo, alisema watuhumiwa wawili waliofikishwa
mahakamani hapo jana, Ruto na mtangazaji wa Redio, Joshua arap Sang wanakabiliwa
na mashtaka matatu kila mmoja, ambayo ni kuwalazimisha watu kukimbia makazi yao,
mauaji na kuchochea ghasia.
Mwendesha Mashtaka wa ICC, Fatou Bensouda alianza kwa
kusoma mashtaka matatu yanayomkabili kiongozi huyo wa Kenya na akaiomba Mahakama
hiyo kumtia hatiani kutokana na vurugu zilizojitokeza baada ya uchaguzi mkuu wa
mwaka 2007.
Akiwasilisha hoja ya mashtaka, Bensouda alisema kuwa
Ruto ni mwanasiasa aliyejawa na kiu ya madaraka na wakati fulani aliitii kiu
yake kwa gharama ya maisha ya wengine.
Alieleza kuwa Ruto alianzisha machafuko alipoona
shabaha yake kutwaa madaraka kwa njia ya kura kushindwa.
“Ruto alikuwa mwanasiasa mwenye nguvu sana ambaye
alikuwa tayari kuratibu uhalifu dhidi ya binadamu ili kukidhi matakwa yake ya
kutwaa madaraka.
"Ni vigumu sana kutathmini maumivu na mateso
waliyoyapata wanaume, wanawake na watoto ambao baadhi yao walichomwa moto huku
macho yao yakishuhudia kile kilichotendeka.
"Wengi waliteswa hadi kufa huku wengine wakitimuliwa
kutoka kwenye nyumba zao na kwenda kuishi uhamishoni,” alisema Bensouda katika
sehemu ya hoja zilizowasilishwa na upande wa
walalamikaji.
Akieleza zaidi mahakamani hapo, Bensouda alisema kuwa
Ruto na wenzake waliapa kutwaa madaraka kwa njia yoyote na walipoona jaribio lao
kwa kuingia Ikulu kwa njia ya kura limeshindikana walianzisha hila kwa kuchochea
machafuko ya kikabila.
Alisema upande wa walalamikaji uko tayari kuthibitisha
madai kwamba Ruto alihusika kuandaa mashambulizi dhidi ya wananchi wa kabila la
Kikuyu.
“Tupo tayari kudhibitisha madai yetu pasipo na shaka
yoyote kwamba mashambulizi ya Wakikuyu yaliratibiwa na kutekelezwa na wahusika
hawa,” alisema Bensouda.
Wakati Bensouda akiendelea kuwasilisha ushahidi upande
wa pili, Ruto alionekana kuwa mtulivu na wakati fulani alitikisa kichwa na kisha
akanyanyua glasi ya maji na kunywa. Kuna wakati pia alitabasamu na kuendelea
kufuatilia kwa makini ushahidi wa upande wa walalamika.
Ruto akana mashtaka
“ Sasa Ruto ni fursa yako kusimama na kujitetea
kuhusiana na mashtaka yaliyopo mbele yako,” alisema mmoja wa majaji kwenye kesi
hiyo. Wakati aliposimama Ruto hakuwa na maneno mengi mbali ya kurudia maneno
yake mara tatu “Sina hatia, sina hatia, sina hatia”.
Ilipowadia zamu ya utetezi wa upande wa washtakiwa,
Mwanasheria wa Ruto, Karim Khan alikosoa vikali maelezo ya walalamikaji
aliyoyaita kuwa ni “uzushi” na baadhi ya washahidi walirubuniwa kwa fedha ili
kutoa ushahidi wa uwongo.
“ Waheshimiwa majaji, najua haki ni muhimu itendeke,
lakini katika hili hakuna ukweli wowote. Sehemu kubwa ya ushahidi uliotolewa na
walalamikaji na hapa singependa nimlalamikie Bensouda kwani ushahidi huu
ulikusanywa na mtangulizi wake Ocampo…hakuna ukweli
wowote.
“ Ushahidi huu umekusanywa bila ya kuwepo mwongozo wa
Mahakama hii waheshimiwa majaji… tena napenda nithibitishe hapa, Ruto ni
mwanasiasa mwadilifu tena mtu safi aliyeletwa kwenye Mahakama hii kwa makosa,”
alisisitiza Khan katika sehemu ya ushahidi wake.
Ili kuonyesha msisitizo wa hoja zake, Mwanasheria Khan
alilazimika kutumia sehemu ya mahojiano yaliyofanywa baina ya Ruto na Mtangazaji
wa K24 Jeff Koinange.
Inakariwa kuwa zaidi ya watu 1,200 walipoteza maisha
wakati wa machafuko hayo ya baada ya uchaguzi na wengine 600,000 walifurumishwa
toka sehemu zao na kwenda kuishi maeneo ya mbali kwa kuhofia usalama wa
maisha.
Taarifa za hivi karibuni zinasema kuwa zaidi ya watu
40,000 bado wanaendelea kuishi kwenye makambi kutokana na makazi yao
kuharibiwa.
Hata hivyo serikali ya Rais Uhuru Kenyatta wiki
iliyopita ilisema kuwa hadi ifikapo Septemba 20 mwaka huu kambi hizo zitakuwa
zimefungwa na wahusika wake watapatiwa msaada wa fedha ili kujenga nyuma
mpya.
Baadhi ya mlolongo wa matukio muhimu kabla ya machafuko
na baada ya machafuko hayo
• Rais Mwai Kibaki alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa
mwezi Desemba 2007 huku mpinzani wake Raila Odinga aliyalalamikia matokeo
hayo
• Vuguvugu la upinzani lilianza rasmi na kufuatiwa na
machafuko yaliyosambaa nchi nzima. Vikosi vya polisi vilikabiliana vikali na
makundi ya waandamanaji.
• Kiasi cha watu 1,200 waliuawa na wengine 600,000
walikimbia nyuma zao
• Uhuru Kenyatta aliyekuwa kwenye kambi ya Kibaki
alishutumiwa kwa kuchochea mapigano dhidi ya wafuasi wa
Odinga.
• William Ruto aliyekuwa kwenye kambi ya Odinga
alilalamikiwa kwa kuchochea mapigano dhidi ya wafuasi wa
Kibaki
• Kilianzishwa majadiliano ya kusaka amani na baadaye
April 2008 mkataba kugawana madaraka ulisainiwa kutokana na majadiliano
yaliyoendeshwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa cKofi
Annan
• Machi 23, 2013 Kenyatta na Ruto waliungana na
kufanikiwa kushinda uchaguzi mkuu
• Septemba 10, kesi dhidi ya Ruto ilianza rasmi wakati
kesi dhidi ya Kenyatta akitazamiwa kuanza Novemba
Macho yake yanapepesa kwa umbali mfupi na kisha
anaelekea moja kwa moja katika chumba maalumu ambacho kimefurika wataalamu wa
sheria.
-Mwananchi
No comments:
Post a Comment