Saturday, August 31, 2013

SERIKALI YASALIMU AMRI YA WABUNGE

bunge_802dc.jpg 
Muswada wa Sheria ya Taifa ya Umwagiliaji wa mwaka 2013, jana ulipita kwa mbinde bungeni mjini Dodoma, huku Serikali ikisalimu amri kwa wabunge na kukubali kurekebisha baadhi ya vifungu vyake.Bila kujali tofauti zao za kisiasa, wabunge jana walisimama kidete na kuonyesha uzalendo wa hali ya juu, wakitaka sheria hiyo imlinde mzawa badala ya mwekezaji.

Moto huo wa wabunge uliwalazimisha Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chizza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema kusalimu amri na kukubali mapendekezo ya wabunge.

Msimamo wa wabunge hao katika kuibana Serikali, pia ulililazimisha Bunge kutengua kanuni zake na kuendelea na shughuli za kupitia muswada huo hadi saa 7:35 mchana, badala ya kusitishwa saa 7:00 kwa ratiba ya kawaida.
Serikali ilikubali mapendekezo ya wabunge hao na kurekebisha vifungu ambavyo sasa vinampa mmiliki wa ardhi itakayotangazwa eneo la umwagiliaji kuwa mwanahisa na kulipwa fidia.

Awali, wabunge waliowasha moto huo ni pamoja na Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina na Suleiman Jaffo wa Kisarawe, wote kutoka Chama Cha Mapinduzi(CCM), ambapo walisema baadhi ya vifungu vya muswada huo wa sheria vilikuwa na ajenda ya siri.

Wakichangia mjadala huo wabunge hao walitaka vifungu vinavyotamka kuwa eneo litakalotangazwa kuwa la umwagiliaji litatwaliwa na Tume itakayoundwa na kupewa fidia viboreshwe, ama kama haifai, vifutwe.

Mpina alishikilia msimamo kuwa badala ya kumlipa fidia mwananchi, vifungu hivyo vitamke kuwa atalipwa fidia ama kuwa mwanahisa wa mradi ama alipwe fidia na papo hapo kuwa mwanahisa.
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), aliitaka Serikali itunge sheria zinazolinda wazawa na kwamba hatua ya kuacha mianya, ndiyo mwanzo wa wawekezaji kuwanyang'anya ardhi wazalendo.

Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka (CCM), alisema kuwa haihitaji kuipitia sheria yote ili kubaini maudhui yenye dhamira ovu dhidi ya Watanzania ndani yake akisisitiza kuwa baadhi ya vifungu vina ajenda ya siri.
"Vifungu hivi vina ajenda ya siri ya kuwapeleka Watanzania kwenye utumwa...Kama msipobadilisha vifungu hivi, mwondoe huu muswada maana hii ni dhambi ya mauti," alisisitiza Ole Sendeka.

Ole Sendeka alisisitiza sheria itamke kuwa kama ni kutwaa ardhi yoyote, hata kama ni Rais anataka kufanya hivyo ni lazima hilo lifanyike kwa ushirikiano na mmiliki wake, ama na wanakijiji wote kupitia mkutano mkuu.
Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya (CCM), alisema Watanzania wameshindwa kunufaika na rasilimali nyingine na waliyobakia nayo ni ardhi hivyo hawako tayari kurudisha ukoloni mamboleo.
Mbunge wa Peramiho, Jenister Mhagama (CCM), alisema ni lazima sheria hiyo iweke sharti la lazima kwa mwekezaji kuingia ubia na mmiliki wa ardhi na kama hataafiki, ndipo apewe fidia.
Chanzo:Mwananchi

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...