Na Boniface Wambura,
IMEWEKWA MEI 19, 2013 SAA 6:20 MCHANA
MECHI ya watani wa jadi Simba na Yanga la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, iliyochezwa jana (Mei 18 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa mabingwa wapya Yanga kushinda mabao 2-0 imeingiza sh. 500,390,000.
Mechi hiyo namba 180 ambayo ilikuwa kati ya saba la kuhitimisha ligi hiyo msimu wa 2012/2013 ilishuhudiwa na watazamaji 57,406 waliokata tiketi kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 30,000.
Kila klabu imepata mgawo wa sh. 123,970,927.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 76,330,677.97.
Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo waliokata tiketi hizo walikuwa 19,039 na kuingiza sh. 95,195,000 wakati kile cha sh. 7,000 kiliingiza watazamaji 17,647 na kupatikana sh. 123,515,000.
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 63,036,064.81, tiketi sh. 3,818,890, gharama za mechi sh. 37,821,638.88, Kamati ya Ligi sh. 37,821,638.88, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 18,910,819.44 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 14,708,415.12.
Ushindi huo leo, umenogesha sherehe za taji la 24 la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa Yanga, kwani mashabiki wa timu hiyo waliangusha bonge la shangwe kuanzia kushangilia mabao hadi taji.
Kwa matokeo hayo, Yanga inamaliza msimu wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 60, ikifuatiwa na Azam FC iliyomaliza na pointi 55 na Simba 45.
Katika mchezo huo, ambao Saanya alisaidiwa na Samuel Mpenzu wa Arusha na Jesse Erasmo kutoka Morogoro, hadi mapumziko Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na Didier Kavumbangu dakika ya tano tu.
Kavumbangu alifunga kwa kichwa akiuwahi mpira wa juu uliopanguliwa na kipa na Nahodha wa Simba, Juma Kaseja kufuatia kona iliyochongwa na Haruna Niyonzima kutoka wingi ya kushoto. Mpira uliozaa kona hiyo ulitokana na Simon Msuva ambaye alikuwa anachanja mbuga, lakini beki Haruna Shamte akatoa nje.
Simba ilipata nafasi ya kusawazisha dakika ya 27 baada ya Mrisho Ngassa kuangushwa kwenye eneo la hatari na Nadir Cannavaro na refa Saanya kuamuru penalti, lakini mkwaju wa Mussa Mudde ulipanguliwa na Ally Mustafa ‘Barthez’ kabla ya kipa huyo kuuchupia na kuudaka.
Kwa ujumla, Yanga ilitawala kipindi cha kwanza karibu chote ingawa mwishoni mwa kipindi hicho, kidogo Haruna Chanongo aliitia majaribioni ngome ya Yanga kama mara mbili hivi na kusababisha kona mbili mfululizo.
Kipindi cha pili, Simba SC walikianza vizuri dakika 10 za mwanzo wakipeleka mashambulizi langoni mwa Yanga kutokea pembeni, lakini safu ya ulinzi ya mabingwa hao wa Bara ilisimama imara kukabiliana na hatari zote.
Krosi maridadi ya Simon Msuva dakika ya 62 iliunganishwa vyema kimiani na Hamisi Kiiza ‘Diego’ kuipatia Yanga bao la pili. Baada ya bao hilo, Yanga sasa walianza kucheza kwa kujiamini zaidi na Simba wakionekana kucheza ili kutoruhusu mabao zaidi.
Dakika ya 87, refa Saanya alijeruhiwa wakati anakwenda kuamua ugomvi kati ya Didier Kavumbangu na Nassor Masoud ‘Chollo’ akaanguka na kutibiwa kwa dakika hadi kuinuka dakika ya 90 na kumaliza mpira baada ya sekunde kadhaa.
Baada ya mchezo huo, kiungo Athumani Iddi ‘Chuji’ wa Yanga alitajwa kuwa mchezaji bora wa mechi na kupewa zawadi ya Sh. 100,000 na wadhamini wa Ligi Kuu, Vodacom.
No comments:
Post a Comment