Sunday, May 05, 2013

MWANAUME AKIKOSA MTOTO HUPATA HUZUNI ZAIDI KULIKO MWANAMKE


Tofauti na mazoea na mtazamo wa wengi kwamba mwanamke ndiye anayeumia zaidi akikosa mtoto, wataalamu wamegundua kuwa anayeumia zaidi kwa kukosa mtoto ni mwanamume.
Utafiti huo umeonyesha kuwa wanaume wanahitaji mtoto sawa sawa na wanavyohitaji wanawake, lakini wao wanaumia zaidi wanapokosa bahati ya kupata mtoto.
Wataalamu hao wamebaini kuwa sababu kubwa zinazowafanya wanaume wajisikie vibaya zaidi wanapokosa watoto ni tamaduni za toka enzi kuwa wao wanaweza kila kitu na msukumo wa familia.
Tofauti na wanawake, ambao wanahitaji mtoto kwa ajili yao binafsi kwa asili ya kuumbwa kwao, hali ambayo kitaalamu inajulikana kama ‘biological urge’.
Taarifa za utafiti huo ulioongozwa na Robin Hadley, wa Chuo Kikuu cha  Keele, ukishirikisha wanaume 27 na wanawake 81, ambao hawajapata mtoto, uliwasilishwa mbele ya Wanasaikolojia wa Taasisi ya British Sociological Association,  ya Uingereza.
Waohitaji zaidi watoto
Kwa idadi hiyo waliosema wanahitaji watoto ni wanaume asilimia 59 na wanawake ni asilimia 63.
Nusu ya wanaume walisema kukosa mtoto kunawafanya waonekane tofauti kwenye jamii, huku wanawake wakisema wanahitaji watoto ili waje kuwasaidia baadaye.
Utafiti huo ulibaini kuwa asilimia 38 ya wanaume walihitaji mtoto kwa kuwa hawakuwa na mtoto kabisa, huku asilimia 27 tu ya wanawake ndiyo walikuwa hawana watoto kabisa.
Utafiti mwingine ulionyesha kuwa wanaume wanajisikia vibaya zaidi kukosa watoto kwa sababu asilimia ya wasio na watoto ni wanaume,tofauti na wanawake ambao wakati mwingine hubahatika kupata mmoja au wawili.
Tafiti hizo zilionyesha kuwa kati ya kila wanaume wanne  mmoja hana kabisa mtoto ikilinganishwa na asilimia 18 ya wanawake ambao hawana watoto.
Utafiti mwingine ulionyesha kuwa asilimia 56 ya wanaume hawana watoto kabisa, ikilinganishwa na asilimia 43 ya wanawake ambao hawana.
Akizungumzia utafiti wake Dk Hadley, anaeleza kwamba  amegundua kuwa kati ya wazazi wawili aliye kwenye hatari ya kukosa mtoto kabisa ni mwanaume, huku akiumia zaidi anapopatwa na hali hiyo kiasi cha kuwa na hasira, kujisikia vibaya mbele za watu, kujitenga na jamii, kuwa na wivu na mambo yanayofanana na hayo.
Wanawake kupenda watoto
Anabainisha kuwa hiyo ndiyo sababu inayowafanya wanawake wapende kupata watoto kuliko wanaume ili kuwaondoa kwenye matatizo hayo, ambayo mara nyingi husababisha familia nyingi kusambaratika bila kujali zilikuwa kwenye maelewano ya kiasi gani.
Alisema kwamba utafiti huo ulifanyika kwa njia ya kukusanya maoni kwenye mtandao, midahalo, kujaza dodoso za majibu na ulihusisha watu wenye umri wa kati ya miaka 20-66 huku wengi waliojibu maswali hayo walikuwa na umri usiopungua miaka 41.
Mtaalamu wa Saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma Modester Kimonga, alisema kuwa kukosa watoto ni tatizo sugu na ndiyo sababu hasa inayowafanya wanawake wahangaike kutafuta tiba ili waweze kupata watoto kwa kuhofia kuharibu nyumba au ndoa zao kutokana na wanaume zao kubadilika.
Alifafanua kuwa kwa mtazamo wa kawaida mwanamke ndiye anayeonekana kuumia zaidi anapokosa mtoto, bila kujua msukumo wa kuhangaika anaoupata kwa mumewe kutokana na anavyomwona au wanavyojadili suala hilo na anavyojisikia vibaya kukosa mtoto.
“Wapo baadhi ya wanaume wanajitahidi kujionyesha hawaumii, lakini wakikaa ndani na wake zao wanawasumbua na wanawake wanaona ni kwa jinsi gani wanavyoumia na ndiyo maana kwa uhalisia wa maisha ya Kiafrika wao ndiyo walengwa mbele ya jamii na huamua kuhangaika kujitibia hospitalini na kwa mitishamba kujitwisha mzigo ambao pengine siyo wao,”alisema Dk Kimonga.
Aliongeza kuwa mwanamume hakubali kushindwa na kwamba kati ya mwanamume na mwanamke, mwenye uwezo wa kubeba aibu na aina yoyote ya manyanyaso kwa kukosa watoto ni mwanamke.
Alisema kuwa licha ya kuongoza kwa kuwanyanyasa wanawake lakini bado wanaume hawana ujasiri wa kuvumilia maisha bila kuwa na mtoto ambapo huona ni aibu na kujitenga na baadhi ya watu, tofauti na wanawake ambao hujichanganya wakiamini wanaweza kupata tiba.
Naye mtaalamu wa Saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(Udsm), Rebeca Sima anasema kuwa kwa tamaduni za Kiafrika mwanaume ndiyo kila kitu katika familia, hivyo ikitokea akakosa mtoto hujiona kama hafai kwenye jamii.
Mwanaume hujiona hana thamani
“Mwanaume hapendi kujiona ana upungufu, hivyo akikosa mtoto hujiona hana thamani. Hali hii huwafanya baadhi yao kuwa walevi wa kupitiliza au wahuni wa kupitiliza wakiamini wanaweza kupata mtoto huko,”anasema Sima na kuongeza:
“Hii hali ya wanaume kujiona wanaweza ipo tangu enzi na enzi na wanaweza kwenda hospitali akaambiwa yeye ndiyo ana tatizo, lakini bado akamshutumu mwanamke kuwa ndiyo tatizo, hata kama ameambiwa hana uwezo wa kupata mtoto. Baadhi yao hujikuta wakianzisha uhusiano nje, ambayo baadaye hupata mimba zisizo za familia kukwepa lawama hizo,”anasema Kimonga.
Anawaasa kina baba kuwa makini na kwenda hatua kwa hatua na wake zao ili kujua tatizo na kulikubali au kulitatua kwa namna sahihi ili kuepuka madhara ikiwamo kuletewa watoto wa nje ya ndoa inapotokea baba ndiyo mwenye tatizo.
Kuwa na tabia tofauti
Kimonga anaongeza kuwa mwanaume asiyekuwa na mtoto huwa na tabia tofauti na zisizo za kawaida na huchagua kimoja kiwe ndiyo sehemu ya maisha yake, kama vile kuwa mlevi kupitiliza, msafi kupitiliza, mcha Mungu kupitiliza, kupenda zaidi muziki.
Henry Urio (35), anasema kuwa ameoa miaka sita iliyopita hadi sasa hajapata mtoto jambo linalomfanya afikirie kuoa mke mwingine, ingawa dini hairuhusu.
“Dini hairuhusu, lakini natamani kuoa mke mwingine ili niweze kupata mtoto, nikishindwa kabisa itabidi niwe na kimada kwani siwezi kuvumilia hali hii. Vijana wenzangu wote wana watoto hasa wa umri wangu wengine hata bado hawajaoa na hwana maisha mazuri kama yangu,”analalamika Urio.
Naye Frenk Yosefu anasema kuwa pamoja na kujisikia vibaya kwa kukosa mtoto inabidi aendelee kuvumilia kwa kuwa tangu aoe miaka saba iliyopita hajawahi kukaa nyumba moja na mkewe kwa zaidi ya siku tatu anafikiri hiyo ndiyo sababu ya kutokuwa na mtoto.

Aliyeachika mara mbili anena
Sikudhani Juma anasema kuwa ameachika mara mbili kwa hiyari yake baada ya maneno kuzidi kuwa hazai, ingawa mumewe wa kwanza inawezekana ndiyo alikuwa na matatizo kwa kuwa yeye ni mke wa pili na umri wake mkubwa na hana mtoto.
Anasema kwa mume wa pili alichoka matusi ya mumewe na mama mkwe wake, hasa mumewe alipozaa na msichana wa nyumba ya nne kutoka kwao,huku wakiishi kifamilia yaani wifi zake shemeji zame na mama mkwe nyumba moja. “Kama sijapata mtoto siolewi tena jamani sitaki kukumbuka nimepata mateso mimi,manyanyaso nimelia karibu siku zote za maisha yangu na sina imani na mtoto wa mume wangu kwa kuwa hafanani na baba yake wala mama yake,”anaonyesha wasi wasi wake Sikudhani.
Alionya kuwa Sikudhani alionya kuwa si vizuri kina baba kuwalaumu kina mama ili kuficha matatizo yao kwa kuwa wengi wao hawaendi kupima na kupata uhakika wa tatizo ni la nani.
Aguster Nchimbi,anasema kuwa baada ya kuteseka kutafuta mtoto kwa muda wa miaka 17, baada ya kufunga ndoa, alipata mtoto, lakini katika kipindi hicho aliyoyapitia yalikuwa ni zaidi ya unyanyasaji ikiwemo kunusurika kutembea na mganga wa kienyeji kwa maelezo ya kupata mtoto. Pia mumewe kuhamia kwa mwanamke mwingine kwa miaka sita na kurudi baada ya kukosa mtoto na huko. Dk Hadley anasema kuwa pamoja na wanaume kupata madhara yote hayo bado hawapendi kuwa na watoto wengi kama wanawake na hilo lilibainika kwenye tafiti ndogo iliyohusisha wanawake na wanaume 125 ambao tayari wana watoto.
Katika utafiti huo asilimia 55 tu ya wanaume ndiyo walikuwa wanataka kuongeza watoto, ukilinganisha na asilimia 59 ya wanawake ambao walikuwa wanahitaji kuongeza.
Mwananchi

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...