Hayo yalielezwa jana jijini Dar es Salaam na muungano wa asasi tano za kiraia uliowakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Elizabeth Missokia.
Kwa niaba ya mitandao hiyo mkurugenzi huyo alisema hakukuwa na haja ya kufuta matokeo hayo na kufanya maboresho kwa kuwa sababu zilizosababisha kufeli kwa wanafunzi zinajulikana na si kama serikali inavyodai kwa sasa.
Missokia alisema kabla ya serikali kutoa uamuzi huo ilitakiwa kuweka wazi mapendekezo ya Tume ya Waziri Mkuu iliyoundwa kuchunguza matokeo hayo ili wadau wa elimu wapate fursa ya kuona sababu zilizochangia kushuka kwa ufaulu katika mitihani hiyo.
“Kwa kufuta matokeo hayo bila wadau kujua sababu na kutoa mchango wao inawaaminisha Watanzania kwamba sababu nyingine hata kama zipo ziliathiri kwa kiwango kidogo matokeo hayo na suala la upangaji wa madaraja kuonekana ni sababu kubwa zaidi kuliko nyingine,” alisema Missokia.
Alisema hiyo sio sababu kwani matokeo ya kidato cha nne yaliyopita huku akiyataja ya mwaka 2009 yalikuwa asilimia 27.5 ya watahiniwa waliopata daraja sifuri, mwaka 2010 sifuri walikuwa 49.6 na mwaka 2011 asilimia 46.4 ambayo ni matokeo mabaya pia.
Alisema kwa mtiririko huo wa matokeo ni lazima kulikuwa na sababu kubwa zaidi iliyochangia kushuka kwa ufaulu na kwamba hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya kubadili utaratibu wa kupanga matokeo na ufaulu duni wa 2012.
Ilielezwa kuwa sababu nyingine ni kutokuwa na walimu wa kutosha hasa kwa masomo ya sayansi; shule kuwa na upungufu mkubwa wa vitabu na vifaa mbalimbali vya kujifunzia na kufundishia; bajeti ya maendeleo shuleni kuwa ndogo; ruzuku mashuleni kufika ikiwa pungufu na wakati mwingine ikiwa imechelewa; mihtasari ya kufundishia ina mkanganyiko mkubwa; na huku mtaala mpya wa mwaka 2005 ukiwa mgeni kwa walimu walio wengi.
“Msingi mbovu wa lugha ya Kiingereza ambayo ndiyo lugha ya mawasiliano darasani; walimu kutokuwa na hamasa ya kufundisha kutokana na madai ya muda mrefu na kufanya kazi katika mazingira magumu sambamba na kukosekana kwa mafunzo kazini ya kuwaimarisha katika ufundishaji wao; na hamasa ndogo miongoni mwa wazazi katika kufuatilia malezi ya watoto wao,” alisema Missokia.
Hata hivyo alieleza kuwa kuandaliwa upya kwa matokeo hayo, serikali inatakiwa ikumbuke kuna athari mbalimbali ambazo zitatokea ikiwa ni pamoja na baadhi ya wanafunzi ambao walijiua baada ya kupata matokeo mabaya.
“Sasa endapo watapata alama za juu nani atakayetakiwa kuwajibishwa kwa hilo?”
Pia kuna baadhi ya wanafunzi na wazazi wameshafanya maamuzi mbalimbali, pamoja na waliokata tamaa na wamepata madhara makubwa kisaikolojia na wengine kukubali kurudia mitihani na kuhoji serikali itatoa fidia gani.
Pia waliwashukia NECTA kutokana na kukanusha kutumika kwa utaratibu mpya wa upangaji wa madaraja huku wakihoji hivyo iliwadanganya Watanzania.
Asasi hizo pia zilieleza kuwa kwa kuwa serikali imeamua kufuta matokeo hayo na hatimaye kupangwa upya kwa utaratibu wa mwaka 2011 zilishauri zoezi hilo kufanyika kwa uwazi kwa kushirikisha wadau wengine wa elimu ili kujiridhisha na uhalali wa alama za wanafunzi zitakazokuwa zinarekebishwa na siyo uchakachuaji katika njia za urekebishaji na upangaji wa matokeo katika madaraja.
CHANZO TANZANIA DAIMA.
No comments:
Post a Comment