Wednesday, May 24, 2017

MBUNGE MSUKUMA AOMBA BUNGE KUCHANGIA RAMBIRAMBI KWA WANAFUNZI WALIOFARIKI GEITA, WABUNGE WENGINE WAZOMEA....!!!

Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Musukuma, ameomba mwongozo akiliomba Bunge liangalie namna ya kuchangia rambirambi kwa wanafunzi watatu waliofariki kwa kuzama Ziwa Victoria.

Kwa mujibu wa Mbunge huyo, Bunge hilo limekuwa na utamaduni wa kuchangia maafa na majanga mbalimbali na kutolea mfano wa ajali iliyoua ya shule ya msingi ya Lucky Vicent Jijini Arusha.

Katika ajali hiyo, wanafunzi 32 walifariki dunia pamoja na watu wengine watatu ambapo wabunge walichanga rambirambi inayofikia Sh86 milioni ambapo ofisi ya Bunge ilichanga Sh14 milioni.

Hata hivyo, wakati Mbunge huyo akiwasilisha mwongozo huo, baadhi ya wabunge wa upinzani walionekana kupaza sauti yao, hadi mwenyekiti Zungu alipolazimika kukemea hali hiyo.

Zungu akitoa mwongozo wake, alisema ni utamaduni wa chombo hicho kuchangia maafa na majanga mbalimbali kama njia za kuonyesha mshikamano na kwamba hilo analichukua atalitolea majibu baadae.

ANGALIA MAJINA YA VIJANA WALIOHITIMU KIDATOCHA SITA WALIOCHAGULIWA KUJIUNGA NA MAFUZO YA JKT KWA MUJIBU WA SHERIA MWAKA 2017

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), limechagua vijana waliohitimu Elimu ya Sekondari Kidato cha Sita kwa mwaka 2017, kutoka Shule zote za Tanzania Bara kuhudhuria mafunzo ya JKT kwa Mujibu wa Sheria.

Sanjari na Uchanguzi huo, JKT limewapangia Makambi watakayokwenda kupatiwa mafunzo kwa muda wa miezi mitatu na wanatakiwa kuripoti Makambini kuanzia tarehe 25 – 30 Mei 2017.

Vijana waliochanguliwa, wamepangiwa katika kambi za JKT Rwamkoma – Mara, JKT Msange – Tabora, JKT Ruvu – Pwani, JKT Makutopora – Dodoma, JKT Mafinga – Iringa, JKT Mlale – Ruvuma, JKT Mgambo na JKT Maramba – Tanga, JKT Makuyuni – Arusha, JKT Bulombora, JKT Kanembwa na JKT Mtabila – Kigoma.

Aidha, wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana kwa macho (physical disabilities) wanatakiwa kuripoti kambi ya JKT Ruvu iliyopo Mlandizi mkoani Pwani ambayo ina miundombinu ya kuhudumia watu wa jamii hiyo.

JKT linawataka vijana hao kuripoti wakiwa na vifaa vifuatavyo:

Bukta ya rangi ya ‘Dark blue’ yenye mpira kiunoni (lastic), iliyo na mfuko mmoja nyuma, urefu unaoishia magotini, isiyo na zipu.

Raba za michezo zenye rangi ya kijani au blue.

    Shuka mbili za kulalia zenye rangi ya blue bahari

    Soksi ndefu za rangi nyeusi.

    Nguo za kuzuia baridi kwa waliopangiwa mikoa yenye baridi.

    Track suit ya rangi ya kijani au blue.

    Nauli ya kwenda makambini na kurudi majumbani.

Mkuu wa JKT anawakaribisha Vijana wote waliochaguliwa ili waweze kujiunga na Vijana wenzao katika kujifunza Uzalendo, Umoja wa Kitaifa, Stadi za kazi, Stadi za maisha na Utayari wa kulijenga na kulitumikia Taifa letu.

Tuesday, May 23, 2017

HUYU NDIYE MWANAFUNZI ALIETUMIA UZOEFU WA KUOGELEA KUWAOKOA WENZIE WASIFE MAJI, GEITA.

Mwanafunzi Tisekwa Gamungu wa shule ya msingi Butwa wilayani Geita, aliyetumia uzoefu wake wa kuogelea kuokoa wenzake tisa baada ya mtumbwi waliokuwa wanasafiria kupinduka jana jioni. Wanafuzni watatu wamepoteza maisha katika ajali hiyo iliyohusisha mtumbwi uliokuwa umewabeba wanafunzi 12.

MIILI YA WANAFUNZI WATATU WALIOZAMA NA MTUMBWI GEITA YAPATIKANA

Wanafunzi watatu kati ya 24 wa shule ya msingi Butwa, waliozama katika ziwa Victoria, kisiwa cha Butwa, wamefariki dunia.

 Awali wanafunzi 21 waliokolewa na watatu hawakuonekana lakini saa chache baadaye, miili mitatu iliopolewa. Ajali hiyo ilitokea jana saa 10 alasiri.

 Mkuu wa Wilaya ya  Geita, Herman Kapufi amesema wanafunzi hao walikuwa kwenye mtumbwi waliotumia kuvuka wakitoka shuleni.

YUSUF MANJI AJIUZULU UENYEKITI YANGA.....!!!

Barua iliyosainiwa na Yusuf Manji Mei 22, 2017 inaonesha kwamba Manji ameachia rasmi nasasi ya uenyekiti wa klabu ya Yanga na makamu mwenyetiki wa klabu hiyo Clement Sanga atakuwa mwenyekiti na kuiongoza klabu hadi hapo uchaguzi utakapofanyika ili kumpata mwenyekiti mpya.

Kwa mujibu wa maelezo ya barua, Manji alifikia uamuzi wa kujiuzulu Mei 20 mwaka huu siku ambayo Yanga ilitangazwa kuwa bingwa wa ligi kuu Tanzania bara 2016/2017.

Katika barua hiyo, Manji amsema ameamua kuachia ngazi ili kutoa nafasi kwa wengine nao kushika uongozi ndani ya klabu hiyo.

Friday, May 19, 2017

UPASUAJI WA MAJERUHI WA AJALI ARUSHA WAFANIKIWA

 Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu anaandika katika ukurasa wake wa factbook kuwa, "Mtoto Doreen amemaliza kufanyiwa upasuaji wa uti wa mgongo, kwa kile ambacho madaktari wamesema kumefanikiwa kwa ufanisi mkubwa, kupita matarajio yao." 

Nyalandu anaeleza zaidi, "Mtoto Doreen alikuwa afanyiwe upasuaji kwa makadrio ya saa 5:30, lakini zoezi hilo lilikamilika kwa muda wa saa 4:00, Huku timu ya "Surgical Support" ikiwa na watu 6 na kwa pamoja wakiongozwa na madaktari bingwa 2, Dk Meyer na Dk Durward."

"Mtoto Doreen amehamishwa kutoka chumba cha upasuaji na kupekewa ICU, na madaktari wamesema kwa kuwa hali yake imeridhisha sana, baadaye leo watamtoa ICU ambako wamempumzisha baada ya upasuaji na kumrudisha wodi yawatoto ambako ataendelea na mapumziko."

DR. SLAA: SINA MPANGO WA KURUDI TANZANIA

ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dr. Willibrod Slaa, amesema hana mpango wa kurudi nchini kwa sasa na kwamba taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii hazina ukweli wowote.

Jana katika mitandao mbalimbali ya kijamii ilisambaa taarifa kwamba mwanasiasa huyo ambaye aliondoka nchini baada ya kujiweka kando na chama chake wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi, angewasili leo nchini.

“Dk. Slaa ataingia kesho (leo) nchini na kwamba atazungumza na waandishi wa habari saa tano asubuhi,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Kutokana na hilo, mwandishi wa habari hii alimtafuta Dr. Slaa kupitia simu yake ya kiganjani akiwa nchini Canada jana, ambapo alieleza kushangazwa na taarifa hizo akisema watu wakikosa ajenda hubaki kutunga mambo.

Thursday, May 18, 2017

SERENGETI BOYS YAWASHIKISHA ADABU WAANGOLA KATIKA MICHUANO YA AFCON U17

Serengeti Boys imefanikiwa kupata ushindi wa kwanza kwenye michuano ya AFCON U17 baada ya kuifunga Angola kwa mabao 2-1 kwenye mchezo wa Kundi B uliochezwa jioni ya leo Alhamisi Mei 18, 2017.

Vijana wa Serengeti Boys ndio walikua wa kwanza kupata bao la kuongoza dakika ya sita kipindi cha kwanza baada ya Kelvin Naftal kupasia kamba kwa kichwa akiunganisha krosi ya Nickson Kibabage.

Dakika ya 18 Angola walisawazisha bao hilo kupitia kwa Pedro baada ya kutumia vizuri makosa ya safu ya ulinzi ya Serengeti Boys na kufanya timu zote kwenda mapumziko zikiwa sare kwa kufungana 1-1.

Kipindi cha pili Serengeti waliongeza kasi kutafuta bao na kufanikiwa kufunga dakika ya 69 mfungaji akiwa ni Abdul Suleiman baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Yohana Mkomola. Mungu ibariki Serengeti Boys, Mungu ibariki Tanzania.

SHILOLE AWATAJA DIAMOND, ZALI KWENYE KESI YAKE

 
MSANII wa Bongo Fleva, Zuwena Mohamed ‘Shilole’, ameieleza mahakama jinsi mwanafunzi wa Chuo cha Bandari, Thomas Lukas, alivyokuwa akitumia mtandao wa kijamii wa Instagram kutuma meseji za matusi ya nguoni kwa watu mbalimbali.

Shilole alitoa ushahidi huo jana katika Mahakama ya Wilaya Kinondoni mbele ya Hakimu, Boniface Lihamwike.

Akiongozwa na wakili wa Serikali, Tumaini Mfikwa, Shilole alidai shughuli zake ni muziki na anatambulika kwa jina la Shilole ama Shishi baby.

Shilole: Mheshimiwa mimi nafanya kazi sehemu nyingi hasa kwenye Instagram, WhatsApp, Facebook na Twitter…, nipo kwenye mitandao hiyo tangu nilipokuwa superstar miaka mitano iliyopita.

Alieleza Shilole huku akidai kwamba mwaka jana alipokea simu za watu tofauti wakiwemo wasanii wenzake na mashabiki wake wakimlalamikia kuhusu meseji za matusi anazowatumia kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Shilole: Yaani mimi kama mwanamke nilidhalilishwa sana na hayo matusi, mheshimiwa Hakimu ukitaka nayataja hapa.
Hakimu: Subiri…
Shilole: Ndipo nikaamua kwenda kituo cha Polisi Osterbay kuonyesha jinsi mtuhumiwa alivyotumia jina langu vibaya.

Hata hivyo, alipotakiwa na Wakili wa utetezi, Julias Kamote na Christina Roman ataje baadhi ya majina ya wasanii waliomlalamikia, aliwataja kwamba ni Queen Darlin, Diamond, Zali, Ant Ezekiel na Harmonize mwingine ni mtangazaji, Efrahim Kibonde.

Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Juni 6, mwaka huu na mtuhumiwa yupo nje kwa dhamana.

TRUMP AIMWAGIA TANZANIA FEDHA ZA KUPAMBANA NA UKIMWI

Serikali ya Marekani kupitia mpango wa dharura wa Rais wa nchi hiyo wa kukabiliana na Ukimwi (Pepfar), umeidhinisha Dola 526 milioni katika kipindi cha mwaka mmoja ujao kwa ajili ya kukabiliana na VVU na Ukimwi nchini.

Msaada huu utaongeza idadi ya Watanzania wanaopatiwa matibabu ya kufubaza VVU kufikia milioni 1.2.

Pia utaimarisha mapambano dhidi ya VVU kupitia huduma za upimaji, matibabu, kufubaza na kuzuia maambukizi ili hatimaye kufikia lengo la kutokomeza Ukimwi ifikapo mwaka 2030.

Taarifa ya ubalozi wa Marekani nchini imesema fedha hizo zitafadhili miradi inayotekelezwa chini mpango wa utekelezaji wa  Pepfar utakaoanza kutekelezwa Oktoba hadi Septemba 2018, na ni ongezeko la asilimia 12.3 ya bajeti ya mwaka jana.

Bajeti iliyotengwa inajumuisha pia utoaji wa huduma na matibabu kwa watoto yatima na walio katika mazingira hatarishi pamoja na kukabiliana na ukatili wa kijinsia.

Pepfar pia itasaidia mpango wa tohara ya hiari kwa wanaume, walengwa wakiwa 890,000.

Mpango huu unaendeleza ubia wa muda mrefu kati ya Marekani na Tanzania katika sekta ya afya ikiwa ni pamoja na muongo mmoja wa ushirikiano uliowezesha kudhibiti kwa mafanikio maambukizi ya VVU.

Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Virginia Blaser alisema, “Kwa pamoja tunafanya kazi ili hatimaye kuwa na kizazi kisicho na Ukimwi Tanzania – ambacho hakuna hata mtu mmoja anayeachwa nyuma.”

MWILI WA MTOTO ALIEPOTEA, WAKUTWA HAUNA MACHO, ULIMI NA MENO MAWILI

Mtoto Felister Isack Skali (7) pichani, ambaye alikuwa mwanafunzi wa chekechea katika Shule ya msingi Mwagala Mbuyuni Wilaya ya Songwe Mkoa wa Songwe aliyetoweka katika mazingira ya kutatanisha tangu mei 11 mwaka huu, mwili wake umekutwa porini ukiwa hauna baadhi ya viungo kama ulimi, macho na meno mawili ya chini.

Akithibitisha kupatikana kwa mwili wa marehemu Afisa Mtendaji wa kijiji cha Mbuyuni Athanas Hamis amesema alipata taarifa kutoka kwa wachungaji wa mifugo ambapo alifika eneo la tukio jioni na wanachi kulazimika kulinda mwili hadi asubuhi walipofika askari Polisi wa kituo cha Galula na Daktari na kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu kisha mazishi kufanyika jana.

Tukio hilo ni la kwanza kutokea katika kijiji cha Mbuyuni ambalo linahusishwa na imani za kishirikina.

Friday, May 05, 2017

UPELELEZI ALIYEJITOSA BAHARINI WAKAMILIKA

Wakati Polisi Zanzibar ikisema imekamilisha kumhoji msichana aliyejitosa Bahari ya Hindi eneo la Chumbe alipokuwa akisafiri na boti ya Kilimanjaro (V) kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar, mtaalamu anasema binti huyo amethirika kisaikolojia ni bora angeachwa apumzike.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Hassan Nassir Ali alimwambia wa habari hii jana kuwa, msichana huyo anayesoma kidato cha tatu Sekondari ya Glorious na watu wengine wameshahojiwa kuhusu tukio hilo la Aprili 3.

Hassan alisema miongoni mwa walihojiwa ni wanafamilia, msichana huyo na manahodha wa boti ya Kilimanjaro ambao walimuokoa.

Alisema polisi imepata taarifa kamili juu ya tukio hilo, hivyo wakati wowote jalada litafikishwa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa hatua zaidi za kisheria.

PENGO APELEKWA MAREKANI KWA MATIBABU

ASKOFU wa Kanisa Katoliki  Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amepelekwa nchini Marekani kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya yake.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari, Dar es Salaam jana na Askofu Msaidizi wa jimbo hilo, Eusebius Nzigilwa alisema Kardinali Pengo alisafirishwa Mei 2, mwaka huu kwa ajili ya kupatiwa matibabu na kufanyiwa uchunguzi.

Alisema Kardinali Pengo, anatarajiwa kuwapo nchini Marekani kwa mwezi mmoja.

“Tuendelee kumuombea Baba Kardinali Pengo ili mwenyezi Mungu amjalie nguvu na afya njema ya mwili na roho ili aweze kuliongoza vema Taifa la Mungu alilokabidhiwa,”alisema  Nzigilwa.

Hivi karibuni, hali ya afya ya Kardinali Pengo, ilionekana kudhoofu kutokana na maradhi yanayomsumbua, kitendo kilichosababisha ashindwe kuongoza misa za ibada kanisani.

Wakati wa misa ya Sikukuu ya Pasaka iliyofanyika hivi karibuni, Kardinali Pengo alionekana kudhoofu na kufikia uamuzi wa kukataa kupigwa picha na waandishi wa habari waliohudhuria misa hiyo.

Thursday, April 20, 2017

TFDA YAPOKEA MAOMBI 767 YA VIWANDA VIPYA

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Chakula na Dawa(TDFA), Hiiti Sillo amesema kuanzia Machi mwaka huu taasisi yake ilimepokea maombi mapya ya usajili wa viwanda 767.

Amesema katika maombi hayo, viwanda 635 vipya vimesajiliwa kati ya hivyo, 613 vya chakula, kimoja cha dawa na 21 vya vipodozi akisema hiyo ni asilimia 82.8 ya maombi yote jambo linaloashiria kwamba waombaji wengi wanazingatia sheria.

Amesema katika kipindi hicho TFDA ilifanya tathmini ya maombi 4,762 sawa na asilimia 82.1 ya usajili wa bidhaa za dawa, chakula, vifaatiba na vipodozi, kati ya maombi 5,802 yaliyowasilishwa na 4,322 (75%) yaliidhinishwa na 440 yalikataliwa kwa kutokidhi vigezo vya ubora.

Sillo ameeleza hayo leo kwenye mkutano na wahariri wa vyombo vya habari walipokutana mkoani Tabora.

'UPINZANI HAUNINYIMI USINGIZI' MUGABE

Viongozi wawili wa vyama vya upinzani nchini Zimbabwe wamekubaliana kuunda umoja kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu ujao nchini humo.

Kiongozi wa Movement for Democratic, Morgan Tsvangirai na aliyekuwa makamu wa rais wa nchi hiyo Joice Mujuru wa National people's Party walitia saini makubaliano hayo siku ya Jumatano.

Rais wa nchi hiyo Robert Mugabe awali alitoa maneno ya dhihaka kutokana na mipango ya upinzani aliyodai kuungana kumuondoa madarakani.
Morgan Tsvangirai na Joice Mujuru wameonekana kumaliza baadhi ya tofauti zao.Tsvangirai anasema makubaliano yaliyotiwa saini baina ya vyama viwili ni msingi kuelekea kuunda umoja wa vyama kwa ajili ya kupambana na chama tawala Zanu PF.

Changamoto iliyopo hivi sasa ni kuamua nani kati ya hao wawili ataongoza muungano huo.

Tayari, vyama vingi vidogo vya upinzani vimemuidhinisha Morgan Tsvangirai kuwa mgombea wao wa urais.

Kiongozi wa miaka mingi madarakani Robert Mugabe , alieleza kuwa upinzani umejaa watu wasio na kitu vichwani.

Amesema hakosi usingizi kwa kile kinachoitwa umoja wa wapinzani.

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...