MWENYEKITI WA CCM DK JAKAYA KIKWETE.
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete amefungua milango kwa kuwataka baadhi ya watu ndani ya chama hicho wanaowania urais mwaka 2015 kuendelea na mchakato huo.
Rais Kikwete amewatahadharisha watu hao kuendesha kampeni zao kwa ustaarabu pasipo kuibua chuki wala kujenga makundi ambayo alisema ni hatari kwa kuwa yanaweza kukipasua chama.
Rais Kikwete aliyasema hayo katika mkutano ndani wa wabunge wa chama hicho uliofanyika jana katika ukumbi wa CCM (white house) mkoani hapa.
Mkutano huo ambao ulianza saa 3.00 asubuhi ulilenga kujadili masuala mbalimbali ya taifa ikiwamo utekelezaki wa ilani ya uchaguzi ya chama hicho katika majimbo na ahadi mbalimbali za viongozi wa taifa.
Chanzo chetu cha habari kutoka ndani ya ukumbi huo kilieleza kuwa Rais Kikwete aliwataka wanachama wenye nia ya kugombea urais kuwa na tahadhari na watu aliowaita vishoka wa siasa.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, Rais Kikwete alisema watu wa aina hiyo wana tabia ya kula huku na huku kwa kujiingiza katika kambi zaidi ya moja.