Mwenyekiti wa Chama cha CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amezungumzia uteuzi wa Dk. Wilbroad Slaa kuwa balozi akisema hakutarajia.
Rais John Magufuli juzi alimteua Dk. Slaa aliyewahi kuwa katibu mkuu wa Chadema kabla ya kukihama chama hicho wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Wakati wa mchakato wa uchaguzi huo, Profesa Lipumba na Dk. Slaa ambao vyama vyao vilikuwa katika umoja uliojulikana Ukawa, walijiondoa baada ya Chadema kumpitisha Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa kuwa mgombea wake wa urais.
Akizungumza na Mwananchi jana, Profesa Lipumba alisema, “Imekuwa kama surprise, sikutegemea kama Dk. Slaa atateuliwa kwa sababu muda mwingi yupo Canada”.
Hata hivyo, Profesa Lipumba alisema hana shaka na uteuzi huo “Narudia, sikutegemea. Ila popote atakapopangiwa kazi Dk. Slaa atafanya kwa sababu najua ni mchapakazi,” alisema.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema Rais Magufuli ana mamlaka kisheria ya kumteua mtu atakayemuona anafaa katika nafasi fulani.