Wednesday, September 06, 2017

WANAFUNZI 917,072 KUFANYA MTIHANI WA DARASA LA SABA LEO

Baraza la Taifa la Mitihani nchini (NECTA) limesema maandalizi ya kuanza mtihani wa Taifa wa darasa la saba utakaofanyika leo jumatano Septemba 6 na kesho alhamisi ya Septemba 7 yamekamilika.

Akizungumza na wanahabari kuhusu maandalizi hayo, Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Charles Msonde. Tayari mitihani imesafirishwa katika maeneo yote nchini na kinachosubiriwa kwa sasa ni kuanza kwa mtihani.

“Leo na kesho katika shule zetu 16,583 za msingi nchini kutakuwa ana mtihani wa kumaliza elimu ya msingi, watahiniwa ni 917,072 wataufanya wavulana wakiwa 432,744 sawa na asilimia 47.19%, wasichana ni 484,328 sawa na asilimia 52.81%, mwaka jana watahiniwa walikuwa 795,761.

EMIRATES TANZANIA YAPATA BOSI MPYA

Uongozi wa shirika la ndege la kimataifa la Emirates umemteua Bwana Rashed Alfajeer kuwa meneja mkuu mpya wa shirika hilo nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa ya msemaji wa shirika hilo nchini Tanzania inasema, Bwana Alfajeer, kutoka katika nchi za Falme za Kiarabu, atakuwa na jukumu la kusimamia shughuli zote za Emirates za kibiashara, wateja na mizigo kwenye soko.

"Nina furaha kwa kuchaguliwa kuwa meneja mpya wa Emirates nchini Tanzania na ninatarajia kufanya kazi na timu ya ndani, pamoja na washirika wetu wa biashara katika kuendeleza biashara zaidi ya Emirates kwenye soko," alisema Alfajeer.

"Mtazamo wangu utakuwa kuendelea kuwapa wateja wetu wa Tanzania huduma bora kulingana na thamani ya pesa, tunapowaunganisha kwenye maeneo zaidi ya 150 ulimwenguni kote," aliongeza.

Bwana Alfajeer alijiunga na Emirates mwaka 2013 kama sehemu ya mpango wa Emirates kama msimamizi wa Taifa wa Uendeshaji wa Biashara. Tangu wakati huo, amefanya kazi za biashara nchini Sri Lanka kabla ya kuchukua nafasi ya Meneja wa Wilaya huko Dammam, Saudi Arabia mwaka 2015.

Emirates hufanya safiri mara moja kwa siku kati ya Dar es Salaam na Dubai na ndege kubwa aina ya Boeing 777.

HASHIM RUNGWE ASHIKILIWA NA POLISI

Aliyekuwa mgombea Urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Hashim Rungwe anashikiliwa na polisi kwa siku nne sasa.

Rungwe ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Chaumma anashikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Kanda Maalumu ya Dar es Salaam. Mwanasiasa huyo anashikiliwa akituhumiwa kughushi nyaraka.

Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema jana Septemba 5 kuwa, Rungwe anashikiliwa kituoni hapo kwa siku nne.

Hata hivyo, Kamanda Mambosasa hakutaka kuingia kwa undani kuhusu suala hilo akisema hana taarifa za kutosha.

JAJI MARAGA AMJIBU UHURU KENYATTA

JAJI Mkuu David Maraga amejibu shutuma kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta na viongozi wengine wa Chama cha Jubilee, kufuatia uamuzi wa  Mahakama ya Juu kufuta matokeo ya uchaguzi wa urais.

Viongozi wa Jubilee wamemkosoa Maraga wakidai anatumiwa na upinzani kutoa maamuzi yanayoupendelea muungano wa NASA, na wameapa  kuupitia uamuzi huo wa mahakama wakati uchaguzi utakapomalizika.

“Mimi si mwanasiasa na ninafanya kazi kwa kuzingatia misingi ya kiapo cha utii nilichoapa kuwatumikia Wakenya. Siungi mkono Jubilee wala NASA au  mtu yeyote,” alisema Jaji Maraga katika taarifa yake fupi jana.

Rais Kenyatta mwishoni mwa wiki iliyopita alimkosoa Maraga akimwita ‘mkora’, kwamba ‘alipindua’ matakwa ya mamilioni ya Wakenya waliomchagua.

Kufuatia vitisho hivyo, ambavyo vimelaaniwa vikali na wanaharakati na katika mitandao ya jamii, Maraga ambaye ni mzee wa Kanisa la Sabato (SDA),  alisisitiza kuwa anamwogopa Mungu pekee.

“Ninafuata katiba yetu. Nendeni mkaendeshe uchaguzi na iwapo mtu anapinga, lete shauri ukiwa na ushahidi mzuri na nitalifanyia kazi ipasavyo.  Kumbuka namhofia Mungu pekee,” alisema Maraga ambaye anaongoza mfumo wa mahakama

Friday, August 18, 2017

MAPACHA WALIOSHIKANA WAFARIKI MUHIMBILI

Pacha walioshikana ambao walikuwa wamelazwa katika hospitali ya taifa ya Muhimbili mjini Dar es Salaam wamefariki kwa mujibu wa msemaji wa hospitali hiyo.

Pacha hao waliokuwa wakifanyiwa vipimo ili kuwaanda kwa upasuaji walifariki siku ya Jumanne kulingana na bi Neema Mwangomo. Watoto hao walizaliwa wilayani Kilosa katika eneo la Morogoro. Familia yao ilitoka katika kijiji cha Chaumbele.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Bi Mwangomo alisema kuwa wataalam watatoa maelezo katika wakati ufaao.

Pacha hao walioshikana chini ya kifua na tumboni walikuwa wakitumia ini moja na mishipa ya moyo lakini kila mmoja alikuwa na tumbo lake.

Awali daktari wa watoto Dkt Zaituni Bokhary alitumai kwamba pacha hao wanaweza kutenganishwa watakapofikisha umri wa miaka sita.

MUGABE: 'WALIOWAUA WAZUNGU HAWATASHITAKIWA'

Rais Robert Mugabe, ameuambia umati wakati wa sherehe za siku ya mashujaa jijini Harare Jumatatu wiki hii kuwa watu waliowaua wakulima wa kizungu wakati wa mabadiliko ya sheria ya ardhi nchini Zimbabwe hawatashtakiwa.

“Ndiyo, tuna wale waliouawa wakati wakipinga ukoloni. Hatuwezi kuwashtaki wale waliowaua wazungu. Je, tutawashtaki vipi?” alisema Mugabe.

Wakati wa ukoloni, ardhi nzuri ilitengwa kwa wazungu, lakini mwaka 2000, Mugabe aliongoza kutwaliwa kwa ardhi hiyo kutoka kwa wakulima 4,000 wa kizungu.

Rais Mugabe awali alikiri kuwa mifumo ya ardhi ya nchi hiyo ilishindwa na mwaka 2015 alisema: “Nafikiri mashamba tuliyowapa watu wetu ni makubwa, hawawezi kuyasimamia.”

Kutwaliwa ghafla mashamba kutoka kwa wakulima wazungu, inaonekana kuwa sababu kuu ya kuporomoka kwa uchumi wa Zimbabwe tangu mwaka 2000.

DANGOTE: 'NIKIINUNUA ARSENAL NITAMFUKUZA WENGER'

Mfanyabiashara tajiri raia wa Nigeria Aliko Dangote, ambaye anaorodheshwa kuwa mtu tajiri zaidi Afrika, amesema kuwa atamfuta kazi meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, ikiwa atafaulu kuinunua klabu hiyo ya Uingereza, kwa mujibu wa shirika la Bloomberg.

Wakati wa mahojiano na shirika hilo, Dangote alisema kuwa atajaribu kuinunua klabu hiyo, wakati ujenzi wa kiwanda chake cha kusafisha mafuta cha gharama ya dola bilioni 11 mjini Lagos utakapokamilika.

Bw. Dangote anasema amekuwa shabiki wa Arsenal tangu mwaka 1980.

Wenger ni mmoja wa mameneja wa kandanda wanaosifika sana barani Ulaya na hivi majuzi, alisaini mkataba wa miaka miwili na kuendelea kuwa na klabu hiyo kwa zaidi ya miongo miwili.

Kuna maoni tofauti kutoka kwa wafuasi wake, wengine wakisema kuwa klabu hiyo inahitaji meneja mpya ili kiweze kurejea hadhi yake.

Friday, August 11, 2017

NI UHURU KENYATTA TENA KENYA

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (IEBC), Wafula Chebukati amemtangaza Rais Uhuru Kenyatta kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais.

Chebukati amemtangaza Kenyatta chama Jubilee kwa kupata kura 8,203,290 sawa na asilimia 54.27 ya kura zote zilizopigwa huku mpinzani wake, Raila Odinga aliyekuwa anawakilisha Muungano wa vyama vya upinzani (NASA), akipata kura 6,762,224 sawa na asilimia 44.74 ya kura zote zilizopigwa.

Aidha, watu waliojitokeza kupiga kura walikuwa 15,073,662 sawa na asilimia 78.91 kati ya milioni 19 waliojiandikisha kupiga kura huku kura zilizoharibika zikiwa 399, 935.



Licha ya mchuano mkali ambao ulionyesha tangu awali Kenyatta akiongoza lakini Raila na wafuasi wake waliamini ameshinda uchaguzi huo huku akitaka tume imtangaze kuwa mshindi wa urais.



SERIKALIYAZIMBAMBWEYAKATAAWAFUNGWA KUPIGA KURA


Serikali ya Zimbabwe imekataa ombi la chama cha MDC-T la kuwaruhusu wafungwa kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo ambao utafanyika mwakani 2018.

Taarifa ambayo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Sheria ya Zimbabwe, Virginia Mabiza imeeleza kuwa hawawezi kuwaruhusu wafungwa kupiga kura kwani sheria za nchi hiyo haziruhusu.

Aisha Mabiza amekishauri chama hicho cha MDC-T kuwa kama inataka wafungwa waruhusiwe kupige kura basi watume maombi katika Bunge la nchi hiyo ili lifanye marekebisho ya kisheria ambayo yatawapa ruhusa wafungwa kupiga kura.

“Ninashauriwa na washauri watu na uamuzi ambao ninauchukua ni ambao unaruhusiwa na sheria ya nchi, na kama ni jambo ambalo linakiuka katiba jambo pekee ambalo linahitajika ni kwenda Bungeni kuomba kubadilisha sheria,” alisema Mabiza.

Thursday, July 20, 2017

RAIS MAGUFULI ATOA SIKU 14 VITUO VYA MAFUTA KUFUNGA MASHINE ZA KIELEKRONIKI


Wamiliki wa vituo vyote vya mafuta nchini Tanzania wamepewa siku 14 kufunga na kuanza kutumia mashine za kielektroniki za kutolea risiti la sivyo wafutiwe leseni.

Rais Magufuli, ambaye ametoa agizo hilo, ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuhakikisha vituo vyote vya mafuta nchini vinatumia mashine hizo ambazo kwa Kiingereza zinafahamika kama Electronic Fiscal Petrol Printer na kusisitiza kuwa wamiliki watakaokiuka agizo hilo vituo vyao vifungwe na kufutiwa leseni.

"Na kwa hili natoa siku 14, wale wenye vituo vya mafuta wote, uwe upo Chato, uwe Biharamulo, uwe Kagera, uwe Dar es Salaam hakikisha una hiyo mashine, ndani ya siku 14," amesema Dkt Magufuli.

Mwishoni mwa wiki Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) ilivifungia vituo vya mafuta kutokana kutotimiza vigezo baada ya kutofunga mashine za kielektroniki kwenye pampu za mafuta.

WAZIRI MKUU AONYA MATAMSHI YA UCHOCHEZI


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema Serikali itawashughulikia watu wote wanaotoa matamshi ya kichochezi nchini bila ya kujali nyadhifa zao.

Amesema ni vema watu wakawa makini na kijiepusha kutoa matamshi ambayo yataathiri mfumo wa maisha kwa wananchi wengine.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana, Julai 19, wakati wa ibada ya mazishi ya mke wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe, Linnah Mwakyembe iliyofanyika wilayani Kyela.

Amesema Serikali haitavumilia kuona baadhi ya watu wakitoa matamshi ambayo hayana tija kwa jamii na badala yake yanalenga kuwavuruga wananchi na kuchochea migogoro.

Tuesday, July 18, 2017

WATAKAOKAIDI MAFUNZO YA JKT KUKIONA

Waziri wa Ulinzi, Dk Hussein Mwinyi amesema vijana ambao watakaidi wito wa kuhudhuria mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria, watakuwa wamekaidi amri halali na majina yao yatapelekwa mamlaka za ajira kwa ajili ya hatua dhidi yao.

Kauli hiyo ameitoa wakati JKT ikiendelea na mchakato wa kufufua kambi tano nchini ili kufanikisha uwezeshaji wa vijana wanaomaliza elimu ya juu ya sekondari kujiunga na jeshi hilo kwa kujitolea na kwa mujibu wa sheria.

Awali, ilikuwa lazima kwa wahitimu wa elimu ya juu ya sekondari na vyuo kujiunga na mafunzo ya mwaka mmoja  JKT kabla ya kuendelea na masomo au kuanza ajira, na baadaye muda ukapunguzwa.

TUNDU LISSU: “SIPENDI KUKAMATWA, MAHABUSU SI PAZURI”

Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu amesema hapendi kukamatwa na vyombo vya dola kwa kuwa mahabusu si mahala pazuri pa kuishi watu hususan wasiokuwa na hatia, hata hivyo amesema kitendo hicho hakitamuogofya na kuzuia harakati zake za kupaza sauti.

Lissu ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na wanahabari kuhusu matukio ya baadhi ya viongozi na wafuasi wa Chadema kukamatwa na vyombo vya dola, na kuwekwa mahabusu.

“Sipendi kukamatwa mahabusu si pazuri, lakini inafikia hatua inabidi uamue kama kwenda machinjioni ukiwa umenyamaza kimya au kuingia huku unapiga kelele mataifa yasikie,” amesema.

Lissu ambaye mpaka sasa ana kesi za jinai takribani nne katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ikiwemo ya uchochezi, amedai kuwa baadhi ya viongozi na watumishi wa umma wako katika hali ya hofu katika utendaji kazi wao, huku akiwataka wananchi kupaza sauti ili hali hiyo iondolewe.

“Hofu kila mahali, mahakamani na hata kwenye utumishi wa umma hakuna aliyeko salama. Viongozi wa dini wako kimya wanadhani wako salama. Tunahitaji kupaza sauti kila mmoja kwa nafasi yake,” amesema.

WANA CCM 202 WAJITOKEZA KUWANIA UONGOZI KIBITI

Wanachama 202 wa CCM wamejitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi wilayani hapa, mkoani Pwani.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii, jana Jumatatu Julai 17, Katibu wa CCM wilayani hapa, Zena Mgaya amesema idadi hiyo ni nje ya idadi ya Wana CCM waliochukua fomu za kugombea nafasi za uongozi wa Kata,Shina na Tawi.

Zena amesema pamoja na kuwepo kwa changamoto kubwa za mauaji ya viongozi mbalimbali wa chama hicho, bado mwitikio wa wanachama kuchukua fomu umekuwa wa kuridhisha hasa kuanzia ngazi ya kata na wilaya.

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...