Saturday, March 11, 2017

SOPHIA SIMBA NA MAKADA WENZIE 11 WATIMULIWA CCM

Chama cha Mapinduzi kimewafukuza makada 12 wa chama hicho wakiwemo wanachama mkongwe kama, Sophia Simba, Ramadhan Madabida na Jesca Msambatavangu.

Wakati wanachama hao wakifukuzwa wengine wanne wamepewa onyo kali,  sita wamevuliwa uongozi na kuwekwa chini ya uangalizi mkali wa miezi 30, huku mwenyekiti wa chama hicho Dodoma, Adam Kimbisa akisamehewa.

 Uamuzi huo umetolewa baada  wa kikao cha Nec kilichofanyika Dodoma leo (Jumamosi) na kuongozwa na mwenyekiti wake, Rais John Magufuli.


 Wengine waliovuliwa uanachama ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni Madenge, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Assa Simba, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara,  Christopher Sanya, Mwenyekiti Mkoa wa Shinyanga Ernest Kwirasa, Mwenyekiti wa Mkoa wa Iringa, Nesta Msabatavunga, Mjumbe wa Halamshauri Kuu (NEC) ya CCM, Ali Sumaye, Mjumbe wa NEC Arumeru, Mathias Manga.

Pia, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Longido Leiza amefukuzwa uanachama pamoja  na Mwenyekiti wa CCM Arusha Mjini, Saileli Molleli, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Gairo, Omary Hawadhi, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Muleba, Mwenyekiti wa CCM Babati, Mwenyekiti wa CCM Wilaya Bunda, Mjumbe wa NEC Gureta.

Waliopewa onyo kali kwa makosa mbalimbali ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Iringa Mjini, Ahmed Kiponza ambaye amepewa onyo kali na kuondolewa madarakani, Mjumbe wa NEC Mkoa wa Singida, Hassa Mzaha, Mwenyekiti wa UWT Gezabulu, Mjumbe wa NEC Kilwa, Ali Mchumo na Mjumbe wa NEC Tunduru, Cheif Kalolo ambaye amevuliwa ujumbe huo na kupewa onyo kali.

WANAOFANYA MAPENZI NA WANAFUNZI KUKAMATWA

Naibu Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo, amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Robert Gabriel, kuwakamata watu wote wanaofanya mapenzi na wanafunzi wa shule za msingi.

Jafo aliyasema hayo juzi wilayani hapa, wakati wa ziara yake ya kutembelea Shule ya Sekondari Mnyuzi na Shule za Msingi za Kilimani na Gereza.

Akiwa kwenye shule hizo, Jafo alikagua na kuridhishwa na thamani ya fedha zilizotumika katika ukarabati wa shule hizo.

Pamoja na hayo, aliwataka viongozi wa wilaya hiyo kutowafumbia macho watu wanaoharibu malengo ya wanafunzi kwa kufanya nao mapenzi.

“Mheshimiwa mkuu wa wilaya, lipo tatizo la wanafunzi wa kike wanaopewa mimba na baadhi ya wanaume.

“Wanaume hao wakamateni, muwaweke ndani kwa sababu hatuwezi kuvumilia vitendo vya aina hiyo kwenye jamii yetu.

“Haiingii akilini kuona wazazi na Serikali wanatumia gharama kubwa kuwasomesha watoto, halafu jitihada hizo zinakwamishwa na waovu fulani, hatuwezi kukubali.

“Sisi kama Serikali, tutahakikisha suala hilo tunalifanyia kazi kwa mapana yake ili liweze kuondoka kwenye jamii kwa sababu tunataka wanafunzi wa kike wasome bila vikwazo,” alisema Jafo.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Robert Gabriel, alimuahidi Jafo kwamba, atafanyia kazi maagizo hayo ili wanafunzi wa kike wasikatishwe masomo yao.

Tuesday, March 07, 2017

YA MH. LISSU KAMA FILAMU VILE

Mambo yanayomtokea kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA) ni kama mchezo wa kuigiza.

Jana, Lissu alianza siku kwa furaha baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu kumuona hana kesi ya kujibu, lakini dakika chache baadaye polisi walimkamata tena, kumhoji na kumuachia kwa dhamana.

Licha ya kashikashi hizo mahakamani na kituo cha polisi, Lissu ameonyesha kuwa na sakata jingine katika uchaguzi wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) baada ya kudai kuwa kuna mkakati unasukwa na baadhi ya mawakili wenzake kutaka kumkwamisha asigombee urais wa chama hicho.

 Baada ya kuachiwa huru, Lissu alikamatwa na polisi akiwa Mahakama ya Kisutu na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi, lakini haikueleweka sababu za kukamatwa kwake.

Lissu alikutana na polisi hao saa 4:00  asubuhi na akaambiwa kuwa anahitajika kituoni, mbunge huyo aliomba aendeshe gari lake mwenyewe ambalo alikuwa nalo Kisutu.
Wakili wake, Fredrick Kihwelo alisema: “Polisi walikubaliana naye na kuingia kwenye gari lake na kuelekea kituoni hapo na walipofika walikaa muda kisha wakaelezwa kuwa, anadaiwa kutoa matamshi yanayoweza kusababisha matatizo ya kidini.”

Alisema Lissu alidaiwa kutoa matamshi hayo akiwa mkoani Dodoma, hivyo baada ya mahojiano aliachiwa kwa dhamana na kutakiwa kuripoti kituoni hapo Machi 13.

Chanzo: Mwananchi.

VIGOGO WA ‘UNGA’ WAHOJIWA

Kazi ya kuchunguza majina 97 yaliyokabidhiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa Kamishna wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, imeanza kufanyiwa kazi kwa vigogo watano waliotajwa kuhojiwa.

Februari 13, Makonda alimkabidhi Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo, Rogers Sianga orodha ya majina 97 ikiwa ni awamu ya tatu ya watuhumiwa wa biashara ya dawa za kulevya.

Kamishna wa Intelijensia wa Mamlaka hiyo, Fredrick Kibula alisema jana kuwa wanawahoji na wanafanya uchunguzi dhidi ya watuhumiwa hao kabla ya kuwafikisha mahakamani.

“Tuna watu muhimu watano wanaotoka katika orodha ile ya mkuu wa mkoa. Tunao kwa ajili ya uchunguzi zaidi na muda ukifika tutawatajia mtawafahamu,” alisema Kamishna Kibula na kuongeza:

“Hatukamati ovyoovyo ni lazima tujiridhishe bila shaka kwamba wahusika wana sifa ya kukamatwa. Pia hatutangazi ingawa tunafanya operesheni za kiuchunguzi ambazo zinafanyika mara kwa mara.”

MAGUFULI AAGIZA TANESCO KUWAKATIA UMEME WASIOLIPA BILI

Rais wa Tanzania John Magufuli jana aliiagiza kampuni ya ugavi wa umeme nchini humo (TANESCO) kuwakatia umeme wateja wote wenye madeni makubwa kwa kampuni hiyo, ikiwemo serikali ya Zanzibar.

Akizungumza kabla ya kuweka jiwe la msingi kwenye kituo kipya cha TANESCO mkoani Mtwara, rais Magufuli alisema kuwa tasisi zote za umma zinapaswa kulipa madeni la sivyo zitakatiwa umeme.

Alisema kuwa serikali ya Zanzibar pekee, kupitia shirika la umeme za Zanzibar (ZECO), ina deni la TANESCO kiasi cha shilingi bilioni 121 za Tanzania.

"Msiogope mnapaswa kukata huduma hii kwa taasisi yoyote ambayo hailipi bili zake. Nataka kumwambia waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo kwamba umeme unapaswa kukatwa hata Ikulu. Nikilala gizani, halafu maafisa wa Ikulu ambao hawajalipa watawajibika na sio wewe. Una hakikisho langu kwa hili.

Saturday, March 04, 2017

NYUMBA YA GWAJIMA YAPIGWA PICHA

Wakili  Peter Kibatala amesema polisi wamepiga picha nyumbani kwa Askofu wa Kanisa la Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima.

Kibatala ambaye ni wakili wa Askofu Gwajima amesema jana kuwa mbali na kupekuwa na kupiga picha kila kona walikwenda katika kanisa lake lililopo Ubungo.

“Waache wafanye yao na sisi tutafanya yetu kisheria. Kwani hatuwezi kuwazuia Polisi kufanya shughuli yao na baada ya kumaliza na sisi tutajua nini cha kufanya,” amesema Kibatala.

Msemaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, David Mngongolwa amesema Gwajima alikwenda jana kuripoti kama alivyoamriwa kufanya hivyo.

Mngongolwa amesema baada ya kuripoti askari walimchukua na kwenda naye nyumbani kwake wakakaa kwa dakika zisizozidi sita na kuondoka naye.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Suzan Kaganda amesema hana taarifa za kukamatwa kwa Gwajima kwa maelezo kuwa alikuwa katika kikao.

Wednesday, March 01, 2017

Friday, February 24, 2017

ZINGATIA: UKIPATA AJALI KWENYE CHOMBO CHA USAFIRI KAMA ABIRIA USIHANGAIKE KUPOTEZA MUDA KUTAFUTA MMILIKI, BALI FANYA HAYA.

 
MARA BAADA YA MATIBABU (Kupata nafuu au kupona)
 
1. NENDA  KATIKA KITUO CHA POLISI iliporipotiwa ajali ilikuweza kupata taarifa kuhusu ajali husika na jinsi ilivyoshughulikiwa. Taarifa hizo ni kama zifuatazo:

(a) Gari husika ilikatiwa bima kampuni gani?
(b) Je, ni hatua gani za kisheria zilizochukuliwa dhidi ya dereva wa gari husika. Kwa mfano alipelekwa mahakamani, kesi inaendelea au imeisha au bado anatafutwa au faili limefungwa. Kwa hatua yoyote kati ya hzo hapo juu kama imechukuliwa na polisi kutakuwa na nyaraka zinazoonesha jambo hilo.
(c) Kama kesi imekwisha, omba nyaraka za kesi hiyo kutoka polisi, zikiwemo nyaraka kuhusu ile gari na kampuni iliyoikatia bima. Baada ya hapo;

2. ANDIKA BARUA  kwenda kwa Meneja Mkuu/ Mkurugenzi au Meneja Madai(Claims Manager) wa kampuni husika ya bima. Ndani ya barua hiyo elezea kidogo ilivyokuwa, uliathirika nini kutokana na ajali au umeathirika nini na unadai nini au kiasi gani. KUMBUKA KWAMBA kiwango cha madhara uliyopata kwa mwili ndicho kitathmini au kutilia uzigo kiasi cha madai unachotaka kampuni ya bima ikulipe.

3. KATIKA BARUA hiyo utapaswa kuambatanisha:
(a)  cheti cha matibabu,
(b) tiketi ya safari (kama bado unayo, kama huna haina tatizo),
(c) Fomu ya polisi (PF 3, PF 115),
(d) Charge sheet na nakala ya hukumu (wengine huzitaka hizi)
(e) mchanganuo wa gharama ulizoingia kwa ajili ya matibabu na,
(f)  viambatanisho vyovyote,mfano picha za ulemavu wako, taarifa ya daktari zaidi ya PF3, kama ipo, ikiwamo gharama za usafiri wa kwenda na kurudi hospitali. Iwapo mhanga wa ajali hiyo amefariki basi itahitajika cheti cha kifo, na uthibitisho wa wewe kuwa msimamizi wa mirathi.
 
VINGINEVYO
Unaweza ukafuata utaratibu namba 1 tu hapo. Yaani ukaenda polisi ukakusanya nayaraka zako zote zinazohusina na hiyo ajali, kisha ukawasiliana na Mwanasheria wako kesi ikaelekea mahakamani. Lakini kesi hiyo haitakuwa dhidi ya KAMPUNI YA BIMA bali kesi itakuwa dhidi ya Mmiliki wa chombo cha usafiri kilichopata ajali au kama chombo kilikuwa kinamilikiwa na kampuni basi itashtakiwa kampuni inayomiliki chombo hicho ambayo jina lake lipo kwenye kadi ya gari.
 
MAKOSA YA WATU WENGI.
Watu wengi sana waliopata ajali hasa kwenye mabasi kama abiria, hukimbilia kwa mmiliki kudai fidia. Jambo ambalo wakifika huko hawapati msaada wowote Zaidi ya kuzungushwa zungushwa tu, kutukanwa, kejeli n ahata saa nyingine kuitiwa mbwa. Hili ni kosa. 

Kama ajali imetokea na iliripotiwa polisi, ina maana polisi wana nyaraka na vielelezo vyote kuhusu hiyo ajali. Kwa hiyo mahala sahihi pa kuanzia ni Polisi na sio kwa MMILIKI. Utarudi kw ammiliki tu ikiwa itakuja kuthibitika kuwa mmiliki hakukatia bima chombo chake au bima inayoonekana kwenye chombo chake ni feki. Hapa sasa kesi itakuwa ni kati yako na mmiliki. 

Na hata kwa utaratibu huu usiende kwa mmiliki. Unachopaswa kufanya ni kutafuta taarifa sahihi za mmiliki huyo, yaani wapi anakaa, kadi ya gari, anwani yake, namba ya gari kisha wewe mwenyewe au kupitia kwa mwanasheria wako peleka kesi ya madai ya fidia mahakamani ukiwa na vielelezo vyote vinavyothibitisha kutokea kwa ajali na madhara uliyoyapata. Ni Imani yangu umeelewa.

Tuesday, February 21, 2017

MBOWE ANASWA NA POLISI

Saa 48 zilizotolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Siro kwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe awe amejisalimisha zimetimia akiwa mikononi mwa jeshi hilo jana jioni.

Kamanda Sirro alitoa muda huo Jumamosi iliyopita akimtaka Mbowe afike Kituo Kikuu cha Polisi, vinginevyo wangemsaka kwa namna ambayo wanaona inafaa.

Mbowe alifikishwa kituoni hapo jana jioni, baada ya kupewa saa 48 kujisalimisha muda ambao mwisho wake ulikuwa jana.

Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Kiongozi wa Upinzani bungeni, alijikuta mikononi mwa polisi akiwa kwenye gari barabarani katika Daraja la Mlalakuwa, lililopo Mikocheni na kufikishwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam.

Kukamatwa kwake, ni baada ya Februari 8 kutajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda katika orodha ya watu 65, waliotakiwa kwende kuhojiwa juu ya dawa za kulevya.

Baada ya Mbowe kupelekwa polisi, Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene alisema mwenyekiti huyo alikuwa kwenye gari akitoka nyumbani kwake Kawe, alikutana na gari la polisi na kutakiwa kusimama. 

Wakili wa Mbowe aliyefuatana naye kituoni hapo, Frederick Kihwelo alisema baada ya kutoka kituoni, zaidi ya polisi 10 walikwenda nyumbani kwake kufanya upekuzi hadi saa 3:10 usiku.

Friday, February 17, 2017

QUEEN DARLEEN AUMIA KUISHI BILA MPENZI

Mwanamuziki anayefanya vizuri akiwa chini ya Lebo ya ‘WCB’, ‘Queen Darleen’ amefunguka kuwa anaumizwa sana na hali ya kuishi bila mpenzi jambo ambalo limekuwa likimuumiza sana katika maisha yake ya sasa maana yeye pia anahitaji kupenda na kupendwa kama walivyo watu wengine.
 
Queen Darleen alisema kuwa, tangu aachane na mzazi mwenziye aliyezaa naye mtoto mmoja wa kike hajawahi kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi jambo ambalo amekuwa akijiuliza bila kupata jibu kuwa linasababishwa na nini.

“Naumizwa na hii hali, kuna wakati huwa nafikiria wanaume wananiogopa au sijui ni kitu gani kinatokea sasa nahitaji kuwa na mpenzi,” alisema Darleen.

NUH MZIWANDA AKESHA AKIOMBA WATOTO MAPACHA

Msanii wa muziki Bongo, Naftal Mlawa ‘Nuh Mziwanda’ amefunguka kuwa anakesha kila siku akimuomba Mungu amjaalie mke wake Nawal ambaye sasa ana mimba ya takriban miezi minne ajifungue watoto mapacha.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii hivi karibuni, Nuh alisema kuitwa baba wawili imekuwa ni ndoto yake ya muda mrefu na anaomba itimie kwa mkewe huyo kipenzi. “Niseme tu wazi kwamba natamani sana mke wangu ajifungue mapacha.

Naamini furaha yangu itakuwa zaidi ikiwa hivyo lakini hata akiwa mmoja pia nitashukuru. Kikubwa naomba mke wangu ajifungue salama ili na sisi tuingie kwenye ulimwengu wa wazazi,” alisema Nuh.

Nuh alifunga ndoa na Nawal mwishoni mwa mwaka jana na ilielezwa kuwa, wakati mwanadada huyo akiolewa alikuwa tayari ameshanasa mimba.

Chanzo: GPL

Thursday, February 16, 2017

MANJI AFIKISHWA MAHAKAMANI, ASOMEWA MASHTAKA NA KUPEWA DHAMANA

Mfanyabiashara maarufu Yusufu Manji amepata dhamana baada ya kusomewa shtaka moja la kutumia dawa za kulevya aina ya heroine.

Manji amesomewa shtaka hilo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu  baada ya wakili wake Alex Mgongolwa kuiomba dhamana na Jamhuri kusema haina pingamizi kwani shtaka hilo linadhaminika.

Hakimu Cyprian Mkeha amesema Manji atakuwa nje kwa dhamana kwa sharti la kusaini  bondi ya dhamana ya Sh10 milioni na awe na mdhamini mmoja ambaye atasaini bondi ya Sh10 milioni.

Amedhaminiwa na Katibu Mkuu wa Yanga Charles Mkwassa.

RIDHIWANI AIBUKA SAKATA LA DAWA ZA KULEVYA

Mbunge wa Chalinze Mh. Ridhiwani Kikwete.

MBUNGE wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete (CCM), amesema suala la mapambano ya dawa za kulevya liachiwe Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya chini ya utendaji kazi wa Kamishna Mkuu, Rogers Sianga, aliyeteuliwa na Rais Dk. John Magufuli hivi karibuni.

Ridhiwani ambaye ni mtoto wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, alitoa kauli hiyo jana katika kipindi cha ‘East Africa Breakfast’ kinachorushwa na Kituo cha East Africa Radio kuanzia saa 11 alfajiri hadi saa 3 asubuhi.

Alisema anafikiri vita hiyo ni jambo jema kwani kwa mtu ambaye mambo hayo hayajamkuta, hawezi kuelewa madhara yake na kwamba nguvu kazi ya taifa imekuwa ikipotea kutokana na utumiaji wa dawa za kulevya.

Thursday, February 09, 2017

TUNDU LISSU AGOMA KULA

Wakati Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu akigoma kula hadi afikishwe mahakamani, wakili wake amepeleka maombi Mahakama Kuu kuomba apewe dhamana baada ya polisi kuendelea kumshikilia kwa siku ya tatu.

Wakili wa mbunge huyo, Peter Kibatala alisema mteja wake amefikia hatua hiyo, baada ya Jeshi la Polisi linalomshikilia kumnyima dhamana bila sababu.

“Hakuna sababu za msingi za kumnyima dhamana na tangu jana Lissu hajala na amesema hatakula hadi afikishwe mahakamani,” alisema Kibatala na kuongeza:

“Kosa analodaiwa kulifanya lilifanyika Januari 4 na hadi Februari 6 ni mwezi, kama ni muda wa kuchunguza kosa hata hati ya mashtaka ingekuwa tayari,” alisema Kibatala.

Alisema mteja wao (Lissu) analalamikia kuanzia ukamatwaji wake ulipoanza, alipokamatwa eneo la Bunge bila Spika kuwa na taarifa.

Kibatala alisema polisi waliokwenda kumkamata aliwatambua njiani na alikamatwa bila kuwapo kibali cha kukamata (arrest warrant).

MAREKANI KUMSAKA MTOTO WA OSAMA BIN LADEN

Marekani imemtaja Hamza ambaye ni mtoto wa kiume wa Osama Bin Laden katika orodha ya Magaidi.

Taarifa kutoka wizara ya ulinzi zinasema Hamza Bin Laden akiwa katika umri wa miaka ishirini amekuwa kiongozi makini wa kundi la Al Qaeda ambao ni wapiganaji wa kundi lililoanzishwa na baba yake.

Taarifa zinasema amekuwa makini katika suala hilo kwa kufuata nyayo za baba yake kwa kujiunga na jihadi na kusambaza ujumbe wa sauti kwa niaba ya kundi la Al Qaeda na kuchochea mashambulizi dhidi ya nchi za Magharibi.

Kwa sasa Atazuiliwa kufanya biashara na wananchi wa Marekani na mali zake zitataifishwa.

Kiongozi mkuu wa usalama wa kundi la Al Qaeda Ibrahim al-Banna ametajwa katika orodha hiyo pia.

Marekani itatoa ofa ya dola Million tano kwa atakayesadia kukamatwa kwa al-Banna.

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...