JUMLA ya watahiniwa 775,729 wanatarajiwa kuanza mtihani wa kumaliza elimu ya msingi utakaofanyika leo na kesho nchi mzima.
Aidha, serikali imesema hakuna mtu yeyote atakayeruhusiwa kumzuia mtahiniwa yeyote kufanya mtihani kwa sababu yoyote ile, hata ikiwa ni kutolipa ada.
Akizungumza jana, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania, Dk Charles Msonde alisema kati ya hao, watahiniwa wavulana ni 361,502 ambao ni sawa na asilimia 46.6 na wasichana ni 414,227 sawa na asilimia 53.4.
Watahiniwa wasioona walioandikishwa kufanya mtihani ni 76, wakiwemo wavulana 49 na wasichana 27 wakati wale wenye uoni hafifu wanaohitaji maandishi makubwa ni 698, wavulana wakiwa ni 330 na wasichana 368.