Na Hudugu Ng'amilo.
Bunge
Maalumu la Katiba linaahirishwa leo baada ya kukutana kwa siku 67 bila
kupitisha hata ibara moja kati ya 240 zilizomo katika Rasimu ya Katiba.
Badala
yake Bunge hilo likiongozwa na Samuel Sitta "Mzee wa Kasi na Viwango"
linaahirishwa hadi Agosti, mwaka huu likiendelea kujadili Sura ya Kwanza
na ya Sita zenye jumla ya Ibara 19, zinazohusu masuala yanayojenga
msingi wa aina ya Muungano unaopendekezwa.
Tume ya
Mabadiliko ya Katiba katika rasimu iliyowasilishwa bungeni na aliyekuwa
Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba ilipendekeza muundo wa shirikisho
lenye serikali tatu, pendekezo ambalo limeligawa Bunge hilo vipande
viwili.
Kutokana
na mgawanyiko huo, kauli zenye utata, kejeli, matusi, dhihaka na ubaguzi
ni mambo yaliyoshika hatamu katika mjadala wa sura hizo mbili, huku
viongozi wa Bunge; Sitta na Makamu wake, Samia Suluhu Hassan wakilaumiwa
kwa kushindwa kudhibiti hali hiyo.
Mwanzoni
mwa wiki hii, Mjumbe wa Bunge hilo, Ezekiah Oluoch alimshutumu Sitta
kwamba ameshindwa kudhibiti nidhamu katika Bunge na kwamba ndiye chanzo
cha kuondoka kwa wajumbe wapatao 200 ambao ni wanachama wa Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa). Tafadhari Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz