JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linamshikilia Mwajuma Hamisi, mkazi wa Yombo Vituka kwa kosa la kukutwa na ngozi mbili za chui kinyume cha sheria, zenye thamani ya sh milioni 11.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamishna wa Polisi wa kanda hiyo, Suleiman Kova, alisema mwanamke huyo alinaswa Januari 18, mwaka huu katika eneo la Yombo Vituka, Wilaya ya Temeke.
Kova alisema mwanamke huyo alinaswa baada ya Ofisa Mhifadhi Wanyamapori mkazi wa Ukonga, kutoa taarifa kituoni hapo kwamba kuna mwananchi anauza ngozi za chui.
Alisema askari walifika eneo la tukio na kumkamata mtuhumiwa na walipompekua chumbani kwake, walimkuta na nyara hizo za serikali.
Wakati huo huo, jeshi hilo limesema limemuua jambazi sugu la uhalifu wa kutumia silaha katika majibizano ya risasi na polisi.
Alisema awali polisi waliweka mtego ili kuyanasa majambazi hayo Januari 22 baada ya kufanya tukio la uporaji wa sh milioni 29 kwa mfanyabiashara wa Mtaa wa Kariakoo, anayejulikana kwa jina la Shanys Abdalla, mkazi wa Mbezi.