Na Mwinyi Sadallah, Mwananchi
Zanzibar. Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana amesema ameamua kuweka kambi Zanzibar, lengo likiwa ni kuimarisha chama hicho na kuhakikisha CCM inarejesha majimbo yake yaliyopotea tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1995.
Kinana aliweka msimamo huo kwenye mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa miaka 37 ya kuzaliwa CCM, uliofanyika uwanja wa Soka Kiembesamaki mjini hapa juzi.
Alisema kambi hiyo itaanza kabla ya Aprili mwaka huu, kwa kufanya ziara kuanzia ngazi ya wadi, jimbo, wilaya hadi mikoa kukagua hali ya kisiasa na kuweka mikakati mipya ya chama hicho kisiwani Zanzibar.
"Nitaanza ziara maalumu kabla ya sherehe za Muungano, mengi nitayazungumza wakati huo ukifika, lengo kubwa ni kuangalia uhai wa chama chetu na kuweka mikakati ya kisiasa kabla ya mwaka," alisema Kinana.
Alisema kazi kubwa ya CCM ni kutekekeza sera na ilani yake ya uchaguzi tofauti na vyama vya upinzani, ambavyo ni mahiri na hodari wa kusema bila ya kuonyesha vitendo.
Katibu Mkuu huyo aliviponda vya upinzani nchini na kwamba, CCM imewaachia kazi ya kusema, yenyewe imekijikita kuwatumia wananchi na kutekeleza majukumu yake ya kisera, mipango na mwongozo.
Kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, Kinana alisema watu waliobeza Mapinduzi hayo hivi sasa wamefedheheka kwa kushuhudia yakitimiza miaka 50 huku taifa likiwana hali ya amani, umoja na mshikamano.
Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-like page ya facebook ya Jambo Tz