Mwenyekiti wa baraza la viongozi wa dini la kupambana na dawa za kulevya nchini Shekhe wa mkoa wa Dar es Salaam Alhad Mussa Salum
BARAZA la Viongozi wa Dini la Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, limetaka Jeshi la Polisi kumpa ulinzi Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, kutokana wa ujasiri alioonesha kupambana na dawa za kulevya.
Kutokana na ujasiri huo, Baraza hilo ambalo Mwenyekiti wake ni Shekhe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, limempongeza Dk Mwakyembe na kusisitiza umuhimu wa ulinzi huo kwake, kwa kuwa vita aliyoanza, inaweza kuhatarisha usalama wake.
Shekhe Salum alisema hayo jana alipozungumza na vyombo vya habari Dar es Salaam, akiongeza kuwa kitendo alichofanya waziri huyo kimeonesha uzalendo, ujasiri na upendo alionao kwa Taifa, alilosema linalochungulia kaburi kutokana na dawa hizo.
Maombi maalumu
Kutokana na ujasiri huo na hatari inayomkabili Dk Mwakyembe, pamoja na kutaka ulinzi wa Polisi, Shekhe Salum pia aliomba viongozi wa dini wa imani zote, kumwombea kwa uthubutu huo. Alisema watampa ushirikiano kwa kuunga mkono juhudi anazoonesha ambazo kwa kiasi kikubwa anaamini zitarejesha heshima ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA).
“Kwa dhati kabisa Baraza linataka mawaziri na viongozi nchini kuiga mfano wake, ili kuliondoa Taifa letu katika sifa mbaya ya dawa za kulevya,” alisema Shekhe Salum.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, viongozi wana uwezo mkubwa wa kujitolea kupambana na dawa hizo, isipokuwa hakuna aliye tayari kuonesha uthubutu wake, suala alilosema kwa kiasi kikubwa limechangia mapambano dhidi ya dawa hizo kutofanikiwa.