SIKU chache baada ya Mahakama ya Kisutu kumwachia mtu aliyedaiwa kumteka na kumtesa kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, serikali imemshukia daktari huyo na kudai ndiye chanzo cha kukwama kwa dola kukamata watu waliomteka.
Jana Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali (DPP), Eliazer Feleshi, alidai kuwa vyombo vya dola vimeshindwa hadi sasa kuwakamata waliohusika katika shambulio hilo kutokana na Dk. Ulimboka kukwepa kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi.
Feleshi ambaye jana aliambatana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema, katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, alidai lawama zinazosukumwa kwa Jeshi la Polisi kwa madai ya kushindwa kuwakamata waliomtendea unyama daktari huyo hazina msingi, kwa kuwa mhusika mwenyewe hajafika polisi, licha ya kuitwa mara nyingi kutoa maelezo.
Alisema kama Dk. Ulimboka angetoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kungekuwa na mafanikio makubwa katika kuwasaka na hata kuwatia mbaroni waliohusika katika unyama huo.
“Kila mara mmekuwa mkilaumu polisi wanashindwa kukamata wahalifu lakini tutakamataje kama wenye ushahidi hawataki kutoa ushirikiano?
Kwa mfano mdogo tu ni ‘ishu’ (suala) ya Dk. Ulimboka, hadi leo hajatoa taarifa lakini polisi wanaendelea kusakamwa na kutukanwa tu,” alisema.
Hata hivyo, wakati Feleshi akitoa kauli hiyo, Dk. Ulimboka katika andiko lake alilolitoa mara tu baada ya kurejea nchini kutoka Afrika Kusini alikopelekwa kwa ajili ya matibabu, alimtaja mtu anayeaminika kuwa mfanyakazi wa Idara ya Usalama wa Taifa, Ramadhani Ighondu, kuwa ndiye aliyemteka na kumtesa.
Ulimboka akimtumia Wakili Nyaronyo Kicheere alisema Ighondu na wenzake ni mhusika mkuu katika unyama aliofanyiwa, kauli ambayo imekanushwa mara kadhaa na serikali.
Mapema wiki hii, raia wa Kenya, Joshua Mulundi, aliyekuwa akikabiliwa na tuhuma za kumteka na kumtesa Dk. Ulimboka aliachiwa na Mahakama ya Kisutu baada ya DPP Feleshi kumfutia shitaka. Hata hivyo Mulundi alikamatwa tena na sasa amefunguliwa mashitaka ya kutoa maelezo ya uongo kwa polisi.