PICHA ya maktaba ikionyesha meli ikizama baharini.
ILE meli maarufu kwa jina la ‘Meli ya Magufuli’ ambayo serikali iliinasa katika eneo lake la bahari ya Hindi ikivua samaki bila ya kibali, imezama baharini, Tanzania Daima Jumatano limebaini.
Habari ambazo gazeti hili limezipata, meli hiyo ambayo ina uwezo wa kuvua samaki kwenye kina kirefu baharini, imezama baada ya wajanja wachache kukata vyuma vyake na kuuza kama chuma chakavu.
Kwa mujibu wa habari hizo, wajanja wamekuwa wakiingia na kukata vyuma vya meli hiyo baada ya serikali kuitelekeza kwa muda mrefu bila uangalizi tangu ilipoitaifisha.
Vyanzo vyetu vya habari vilipasha kuwa vyuma chakavu vya meli hiyo vimekuwa vikiuzwa kwa kampuni zinazonunua na kuvisafirisha nje ya nchi na kujiingizia mabilioni ya fedha.
Sehemu kubwa ya vyuma chakavu kutoka kwenye meli hiyo, vimeuzwa kwa kampuni moja inayomilikiwa na mmoja wa wabunge wa Jamhuri ya Muungano.
Inaelezwa kuwa sehemu kubwa ya meli hiyo imetengenezwa kwa malighafi aina ya Brass ambayo kilo moja kwa sasa inauzwa kwa sh 5,200.
Malighafi nyingine zilizotumika na bei yake kwa kilo kwenye mabano vikuzwa kama chuma chakavu ni Cast Aluminum (sh 1,700), Stainless (sh 1,500) na Soft (sh 2,000).