Rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela kulia na rais wa sasa Jacob Zuma
Rais
wa Afrika Kusini Jacob Zuma amesema kuwa afya ya rais wa zamani wa
taifa hilo Nelson Mandela imeanza kuimarika kidogo kutokana na matibabu
anayopewa na Madaktari wake jijini Pretoria.
Zuma
amewaambia wabunge kuwa Mandela anayefahamika kwa jina maarufu kama
Madiba ameanza kuimarika na ni habari njema kwa raia wa nchi hiyo ambao
wamekuwa wakikumbwa na wasiwasi kutokana na afya yake kuendelea
kudorora.
Rais
huyo ameongeza kuwa kila mmoja anakumbuka mchango wa Mandela ambaye
alifungwa jela miaka 27 akiwa katika harakati za kupinga ubaguzi wa
rangi nchini humo na baadaye kufanikiwa kuwa kiongozi wa kwanza mweusi
nchini humo mwaka 1994.
Kiongozi
huyo wa Afrika Kusini amewataka raia wa nchi hiyo na dunia nzima
kuendelea kumwombea Mandela ili apate nafuu haraka na kuruhisiwa kurudi
nyumbani.
Familia
ya Mandela imesema kuwa imeguswa mno na salamu za heri njema
zinazotumwa na watu mbalimbali duniani kumtakia kiongozi huyo wa zamani
nafuu ya haraka.
Mandela
mwenye umri wa miaka 94 alilazwa hospitalini Jumamosi iliyopita baada
ya kuanza kusumbuliwa na mapafu tatizo ambalo limemsumbua kwa muda
mrefu.