HOTUBA
YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI MHE. EZEKIAH DIBOGO
WENJE (MB) KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA MAMBO YA
NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014
1.0 UTANGULIZI
Mheshimiwa
Spika, katika hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
katika bajeti ya wizara hii mwaka 2012/13, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inayoongozwa na CHADEMA ilibaini mapungufu mengi ya kiutendaji
na kiuwajibikaji katika wizara hii, na hivyo kuitaka Serikali kufanya
mambo yafuatayo ili kuboresha utendaji na ufanisi:
1. Kuziwezesha balozi zetu nje kwa kuzitengea fedha za kutosha ili ziweze kufanya kazi kwa ufanisi
2.
Kutoa idadi ya majengo ya balozi zetu nje (nyumba za mabalozi, nyumba
za maafisa wa balozi na ofisi za balozi) kwa mchanganuo wa idadi ya
nyumba katika nchi na kama nyumba hizo zina hati miliki au la.
3.
Kutoa taarifa ya namna kila ubalozi ulivyotekeleza sera ya Diplomasia
ya uchumi kwa kuzingatia kwamba balozi nyingi ziko hoi kifedha kiasi cha
kwamba waambata wa kiuchumi wanakosa fedha za kusafiri kutoka sehemu
moja hadi nyingine kwa ajili ya upelelezi wa masuala ya kiuchumi.
4.
Kulikarabati jengo la ubalozi wa Tanzania huko Msumbiji lililokuwa
limechakaa kwa kutofanyiwa ukarabati tangu 1975 ingawa jengo hilo
tulipewa bure na Serikali ya Msumbiji chini ya FRELIMO.