Jopo la mawakili wanaomtetea Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare leo linaanza harakati za kumtoa mahabusu kwa dhamana.
Hatua hiyo inatokana na uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kumfutia Lwakatare mashtaka ya ugaidi yaliyokuwa yakimkabili yeye na mwenzake Joseph Ludovick Rwezaura, ambayo hayana dhamana na kubaki na shtaka moja la kula njama ambalo linadhaminika.
Kesi hiyo namba 6 ya mwaka 2013, inayosikilizwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, inatajwa leo, lakini mawakili wa Lwakatare wamejipanga kumwombea dhamana Lwakatare.
Mmoja wa mawakili wa Lwakatare, Peter Kibatala aliliambia Mwananchi jana kuwa kwa kuwa kosa lililobaki linadhaminika, basi jambo moja watakalolifanya leo ni kuwasilisha maombi ya dhamana.