Jana
na leo, Serikali imeona kuzuka kwa tabia ya uvunjaji wa kanuni ya
utunzaji wa siri za taarifa za mawasiliano binafsi ya watumiaji wa
huduma za simu za mkononi. Taarifa hizo zimefikia hatua ya kuchapishwa
katika vyombo vya habari kwa kutaja bila idhini yao, namba za simu,
wahusika wa namba hizo, maongezi na muda wa mawasiliano Kati yao. Jambo
hili ni Kosa la Jinai. Mfano; tamko la Chadema lililotolewa na Ndugu
Mabare Marando Mjini Dar es Salaam tarehe 14/04/2013.
Serekali inapenda kuchukua fursa hii kuwakumbusha wenye makampuni ya
Simu, Vyombo vya Habari na wananchi kwa ujumla kuwa, kutoa taarifa za
mawasiliano binafsi ya simu baina ya watumiaji wa huduma hiyo, ni
uvunjaji wa Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta Na. 3 ya
mwaka 2010 na Kanuni za Mawasiliano (Kulinda Wateja) za mwaka 2005.
Kifungu cha 98 ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta
kinasema;
“Mtu yeyote ambaye ni mfanyakazi wa kampuni yenye leseni ya kutoa
huduma za mawasiliano, au mwakilishi wake, ana wajibu wa kutunza siri za
mawasiliano binafsi na taarifa zozote za siri za wateja kwa mujibu wa
sheria hii”. Aidha, “Mtu yeyote haruhusiwi kutoa taarifa binafsi za
mteja yeyote alizopokea au kusikia kwa mujibu wa sheria hii isipokuwa tu
mtu huyo ameruhusiwa kwa mujibu wa sheria”