WANASIASA
wawili vijana ambao wamekuwa katika vita ya maneno na Naibu Katibu Mkuu
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe, kuhusu
madai waliyoyatoa kuwa anawindwa kuuawa, mwishoni mwa wiki iliyopita,
walijitokeza katika ofisi za Mtanzania Jumatano na kufunua siri na
matukio ya utesaji raia na mauaji ya kinyama ambayo yamekuwa yakitokea
kwa nyakati tofauti kwenye shughuli za kisiasa hapa nchini.
Wanasiasa
hao, Juliana Shonza na Mtela Mwampamba, ambao wamefanya mahojiano ya
ana kwa ana na gazeti hili, walisema madai waliyoyatoa awali kuwa Katibu
Mkuu wa Chadema, Dk. Willbrod Slaa, alitajwa na kada wa chama hicho,
Ben Saanane, kuwa alimtuma amuwekee sumu Zitto kwa lengo la kumuua ni ya
kweli kwa sababu walimkamata akiwa nayo na alikiri jambo hilo na
kumuomba msamaha Zitto kwa kitendo hicho.
Walidai,
mbali na tukio hilo ambalo baada ya kuliibua limegusa hisia za wengi na
kuzua mijadala mikali, yapo matukio mengine ya mauaji na majaribio ya
kuua, ambayo yamekuwa yakiratibiwa na Chadema kwa lengo la
kuwagombanisha wananchi na Serikali.
Shonza
na Mwampamba walisema kuwa wapo tayari kutoa ushuhuda wa matukio hayo
mahali popote watakapohitajika na walipoulizwa ni kwa nini baada ya
kubaini kuwepo kwa vitendo hivyo, hawakutoa taarifa kwa vyombo vya
sheria au taasisi za ulinzi na usalama, walisema mlengwa mkuu katika
matukio hayo ambayo yalikuwa yakisababisha madhara kwa watu wengine
hakuwa tayari siri hiyo kuanikwa.