Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, January Makamba amesema uwajibikaji katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne haukuwa wa kuridhisha kwa sababu kulikuwa na utamaduni wa kuoneana haya, kujuana, kusitiriana na kutoogopa.
Amesema hayo yalikuwa yakitokea kwa kuwa waliokuwa wakifanya makosa hawakuwa wakichukuliwa hatua na hivyo kujengeka utamaduni wa watu kutoogopa, lakini sasa utawala mpya umeonyesha kuchukua hatua dhidi bila ya woga.
Makamba, ambaye aliingia tano bora ya mbio za urais ndani ya CCM kabla ya kuangushwa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu, alitoa kauli hiyo juzi katika mahojiano maalumu na Mwananchi ofisini kwake jijini Dar es Salaam juzi.
Alikuwa akijibu swali kuhusu hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa na Serikali ya Rais John Magufuli dhidi ya wakwepa kodi, wabadhirifu, watendaji wazembe na wezi wa mali za umma, tofauti na utawala uliopita wa Serikali ya Awamu ya Nne.
“Nadhani moja ya changamoto zilizosababisha huko nyuma tusifanikiwe sana katika suala la uwajibikaji, ni hili suala la kuoneana haya. Ni hili suala la kuweka kujuana kidogo na ni hili suala la kusitiriana,” alisema Makamba, ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kwenye utawala uliopita.
“Na ukijengeka huo utamaduni na ukajikita mizizi, hatua hazitakuwa zinachukuliwa dhidi ya watu wanaofanya makosa.”
Udhaifu katika kuchukulia hatua watumishi wanaofanya makosa ulikuwa kilio kikubwa cha wanasiasa dhidi ya utawala uliopita na wakati fulani katibu mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana aliwahi kusema kuwa Serikali ni dhaifu kwa kuwa inasitasita katika kuchukua uamuzi.
Wakati fulani, mbunge wa Ubungo (kabla ya jimbo kugawanywa), John Mnyika alikwenda mbali zaidi na kusema kiongozi wa Serikali ndiye dhaifu kwa kuwa Katiba inampa haki ya kutosikiliza ushauri wa mtu wala chombo chochote iwapo ataona hivyo.
Utumbuaji majipu
Lakini tangu Novemba 5, 2015 wakati Magufuli alipoapishwa, takribani watumishi 160 wa Serikali wameshasimamishwa kazi au uteuzi wao kutenguliwa kutokana na kutuhumiwa kuhusika katika ubadhirifu wa fedha za umma, kufanikisha ukwepaji kodi, uzembe na wizi.
“Kwa hiyo kila kiongozi ana staili yake ya namna ya kufanya, lakini mimi kimsingi—kwa sababu hizi kazi ni za umma si kazi zetu binafsi—kimsingi sioni tatizo watu kuambiana ukweli na kama mtu anadhani kwamba ameonewa basi fursa zipo za kutafuta haki yake kutokana na hayo ambayo anadhani kwamba hayajakaa vizuri.
“Kikubwa tu ambacho mimi naamini kinafanyika na kilihitajika ni kujenga utamaduni mpya wa watu kuogopa na kuheshimu wajibu wao, na kwamba hizi kazi si kazi zetu za kudumu. Wakati wowote unapofanya makosa basi kuna mamlaka ya kukuchukulia hatua. Na kwamba kule nyuma ambako watu hawakuwa wanaogopa kabisa, huo si utamaduni ambao kwa kweli ulikuwa unafaa katika kujenga taifa jipya.”
Akizungumzia lawama kuwa staili hiyo ya kutumbua majipu inafanywa kwa kuumbua watu na kwamba makosa hayo yalishafanyika tangu utawala uliopita bila kuchukuliwa hatua, Makamba alisema kosa linapobainika wakati wowote lazima lichukuliwe hatua.
“Kama huko nyuma hakukuwa na utashi wala mifumo ya kuwezesha makosa hayo kubainika, lakini utashi huo upo sasa, basi hatua zichukuliwe,” alisema Makamba ambaye ni mtoto wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba.
“Kila kiongozi ana staili yake na Rais Magufuli amekuja na ujasiri na anataka kujenga nidhamu mpya kwenye nchi,” alisema Makamba.
“Hana deni na mtu. Hii ni falsafa na dira ambayo kiongozi anataka nchi iende kulingana na anavyotaka kuitengeneza. Ni jambo jema kwa sisi tunaomsaidia serikalini na ndani ya CCM.”
Akizungumzia hatua za kuwasimamisha kazi watendaji kwa tuhuma mbalimbali, alisema urais ni taasisi na kwamba kiongozi huyo wa nchi anapotoa amri ya kukamatwa au kufukuzwa kwa mtendaji hakurupuki.
“Nyuma yake kuna mfumo uliomsaidia kuchukua uamuzi huo. Wanaochukuliwa hatua, sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma zinakuwa zimefuatwa,” alisema.
Kuhusu watendaji kusimamishwa kazi ndani ya vikao au katika ziara za mawaziri, huku baadhi wakiwa wamefanya makosa hayo miaka mitano iliyopita, Makamba alisema: “Sidhani kama kuna ukomo wa uharamu wa kosa, kwamba kwa sababu ulifanya kosa mwaka 2012 likibainika mwaka 2015 si kosa tena. Mantiki hii sikubaliani nayo.”
Alisema mtu aliyefanya kosa miaka mitano iliyopita, likibainika sasa na ushahidi ukapatikana lazima achukuliwe hatua.
Bomoabomoa
Kuhusu utekelezaji wa kubomoa nyumba zilizojengwa mabondeni, Makamba alisema utaratibu huo ulikuwepo katika awamu zote nne zilizopita, lakini tatizo sheria za utekelezaji wake hazikuwa zikifuatwa kikamilifu.
“Bonde la Msimbazi lilitangazwa kuwa eneo hatarishi kwa maisha ya watu tangu mwaka 1949 na baadaye mwaka 1979. Kumekuwa na taratibu za kuondoa watu ili kurejesha maeneo hayo katika hali ya yake ya asili,” alisema.
Alisema Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi iliwahi kutangaza Bonde la Msimbazi kuwa eneo maalum ma mipango miji, ili kutimiza suala hilo ilikuwa lazima watu waondolewe.
Alisema kazi ya kuwaondoa wananchi wanaoishi kwenye bonde hilo ilikumbwa na changamoto kadhaa na kukajengeka dhana kuwa wanaonewa.
“Serikali tulieleza kama mtu alipewa kibali na Serikali akajenga nyumba, basi Serikali ilifanya makosa na itamtafutia mahali pengine. Ila kama mtu alikuja tu na kujenga nyumba eneo hilo lazima aondoke,” alisema Makamba.
Alisema waliovamia mabondeni na kujenga, Serikali haiwezi kuweka utaratibu wa kuwapatia maeneo mengine kwa sababu kufanya hivyo ni sawa sawa na kuwapa zawadi wanaovunja sheria.
Alisema licha watu hao kujenga nyumba zao mpaka kufikia hatua ya kuanza kuishi, haiwezi kuwa kipimo cha kujipambanua kuwa hawana makosa.
“Unapofanya makosa ukamilifu wa kosa siyo msamaha kwa kutorekebishwa. Ukisema kwa sababu mtu hakukamatwa wakati akijenga msingi, basi asikamatwe kwa sababu nyumba imeisha si kweli,” alisema.
Alisema kazi ya kubomoa nyumba zilizopo mabondeni iliingiliwa na wanasiasa na akasisitiza kuwa maisha wanayoishi wananchi katika maeneo hayo, si ya kuridhisha na ukiwa kiongozi huwezi kukubali kuona wakiendelea kuishi humo.
“Sisi ambacho tumekubali lazima tuliendeshe zoezi lile kwa utaratibu mzuri zaidi. Lazima watu wapate taarifa na waliovamia kuelezwa wazi kuwa hawatapata stahiki yoyote na waliopewa vibali na Serikali wapewe maeneo mengine,” alisema Makamba.
“Kuna utamaduni ulijengeka kwa muda mrefu wa watu kutoheshimu na kutii sheria. Sasa tukiendelea hivyo hivyo si sawa maana bila sheria hakuna Serikali. Nchi hii mtu hawezi kuamua kujenga kibanda popote na akiondolewa Serikali ndiyo ionekane ina dhambi. Hatuwezi kuendesha nchi kwa utaratibu huu.”
Lakini Makamba alikanusha kwamba Serikali ilitekeleza ubomoaji huo kwa kuwa ilishajihakikishia ushindi kwenye Uchaguzi Mkuu.
“Niseme zoezi hili ni endelevu na limeanza kabla ya Serikali kuingia madarakani. Ila pia nyakati za kufanya maamuzi mazito ni nyakati za mwanzo za utawala mpya,” alisema.
“Magufuli ni Rais anayependa sheria za nchi zifuatwe na utekelezaji wa sheria hizo usilete mzozo na vurugu. Tumekaa na kukubaliana namna nzuri ya kufanya jambo hili. Walioenda mahakamani tutasubiri maana zuio la mahakama linahusu sehemu tu ya eneo si bonde zima. Kwingine tunakoweza kufanya tutaendelea.”
Na Mwananchi
No comments:
Post a Comment