Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila. PICHA|MAKTABA
KATIKA hali ya kushangaza, Mahakama Kuu, Kitengo cha Biashara
imewazuia waandishi wa habari kuingia mahakamani kusikiliza maombi ya
kampuni ya Pan Africa Power Solutions (PAP) na Kampuni ya Independent
Power Tanzania (IPTL) kwa Bodi ya Rufaa ya Kodi nchini, kutaka Kamishna
Mkuu wa TRA akamatwe na kupelekwa gerezani.
Waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari nchini, waliofika
mahakamani hapo jana kusikiliza maombi hayo, walishindwa kusikiliza
kinachoendelea baada ya kuambiwa kuwa waandishi wamezuiwa kusikiliza.
Mmoja wa makarani wa mahakama hiyo, aliwaambia waandishi wa habari
kuwa hawaruhusiwi kusikiliza maombi hayo, lakini hakuwaeleza sababu. Asante
kwa kutembelea blog hii na endelea kuwa nasi siku zote, ukitaka kuwa wa kwanza
kupata habari zetu Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya
neno Jambo Tz
Maombi yenyewe Juzi PAP na IPTL ziliwasilisha maombi kwa Bodi ya
Rufaa ya Kodi (TRAB) zikitaka iamuru Kamishna Mkuu wa TRA, akamatwe kwa
kukiuka amri wa Bodi hiyo iliyozuia kufuta hati za kuthibitisha ulipaji
wa kodi wa kampuni hiyo, katika mauzo ya hisa za IPTL.
Hatua ya TRA kufuta hati hizo ilitokana na madai kwamba PAP ilifanya
udanganyifu kwa kuwasilisha nyaraka za kughushi za ununuzi wa hisa,
zinazodaiwa kuiwezesha kukwepa kodi ya Sh bilioni 8.68.
Maombi ya kampuni hiyo inayomilikiwa na Harbinder Singh Seith,
yaliwasilishwa chini ya hati ya dharura, yakiambatana na kiapo cha
Mkurugenzi Mwendeshaji wa IPTL, Parthiban Chandrasakaran.
Kamishna Mkuu wa TRA anadaiwa kukaidi amri halali iliyotolewa na bodi
hiyo Novemba 26 mwaka huu, iliyozuia kwa muda kuziondoa hati hizo.
“Tunaomba bodi imwamuru Kamishna Mkuu wa TRA kutekeleza amri
iliyotolewa, pia bodi itoe amri ya kuondoa barua ya Kamishna ya Novemba
27 mwaka huu ambayo ilifuta hati za kodi, mpaka maombi ya msingi
yatakaposikilizwa,” ilidai hati hiyo ya maombi.
Hati za PAP zilizofutwa zilitolewa kwa ajili ya uuzaji wa hisa saba
za IPTL kutoka Kampuni ya Mechmar kwenda Piper Links Investment, na
ununuzi mwingine wa hisa hizo hizo kutoka kampuni ya Piper Links kwenda
PAP.
Historia ya hati Katika hati hiyo ya kiapo, Chandrasakaran alidai
Desemba 23 mwaka jana walipata hati hizo za kuthibitisha walilipa kodi
kwa ajili ya uuzwaji wa hisa hizo.
Anadai kwamba Novemba 19, walalamikiwa (TRA) walitoa taarifa ya siku
sita kwa BRELA wakionesha nia ya kuziondoa hati hizo, kwa mazingira
kwamba walalamikaji walipata mkataba feki wa mauzo ya hisa hizo.
“Kamishna si tu anabanwa na mamlaka, pia anatakiwa kufuata sheria za
nchi zikiwamo za bodi, kwa kukiuka amri anapoteza sifa za kuendelea
kushikilia nyadhifa hiyo aliyonayo,” alidai Chandrasakaran katika hati
ya kiapo.
Hata hivyo, kutokana na maombi hayo kuwasilishwa chini ya hati ya
dharura, bodi hiyo mbele ya Katibu wake, Respicius Mwijage iliamuru
yasikilizwe jana, lakini waandishi wakatimuliwa.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila
(NCCR-Mageuzi), ameelezea kushangazwa na madai ya Seith, aliyokaririwa
hivi karibuni katika vyombo vya habari, kuwa suala la Akaunti ya Tegeta
Escrow na umiliki wa Kampuni ya IPTL lilivyoendeshwa na Bunge,
limesababisha atafakari kama ataendelea kuwekeza Tanzania au la.
Akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya NCCRMageuzi jana,
Kafulila alidai kuwa Seith hapaswi kutafakari kwa kuwa yeye sio
mwekezaji na anapaswa kukamatwa na vyombo vya dola, kujieleza namna
alivyonunua IPTL.
“ Ripoti ya CAG imebainisha wazi kuwa Seith alinunua IPTL kwa nyaraka
za kughushi ambalo ni kosa la jinai,” alisema. Hata hivyo, Seith
amekuwa akisisitiza kuwa ununuzi ulifanywa kwa kihalali bila kukiuka
sheria.
Aidha, Kafulila pia alisema NCCR-Mageuzi, imeanza tena ziara mkoani
Kigoma kuendeleza kampeni zake za kuhamasisha wananchi kupigia kura
viongozi wa chama hicho, katika uchaguzi wa serikali za mitaa
unaotarajia kufanyika Jumapili ya wiki ijao.
Kafulila anasema kampeni hizo zinaanza kesho hadi wakati wa uchaguzi
na NCCR itatumia fursa hiyo kuwahabarisha wananchi kuhusu sakata la
Akaunti ya Tegeta Escrow na umiliki wa Kampuni ya IPTL. Asante
kwa kutembelea blog hii na endelea kuwa nasi siku zote, ukitaka kuwa wa kwanza
kupata habari zetu Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya
neno Jambo Tz
Na Habari Leo
No comments:
Post a Comment