Uongozi wa klabu ya Young Africans SC
umempatia taarifa (Notice) ya siku ya thelathini (30) kocha mkuu
mholanzi Ernie Brandts juu ya kusitisha mkataba wake kuanzia jana
Disemba 22 mwaka huu.
Maamuzi hayo yanafuatia muenendo wa
matokeo mabaya katika michezo iliyopita ya Ligi Kuu, kirafiki na bonanza
la Nani Mtani Jembe dhidi ya Simba SC mwishoni mwa wiki.
Hatua ya Young Africans SC kusitisha
huduma na Brandts isichukuliwe kama chuki bali ni moja ya sehemu ya
kuhakikisha tunaboresha benchi la ufundi ili tuweze kupata matokeo
mazuri katika Mashindano yanayotukabili.
Ukitazama uwezo wa mchezaji mmoja
mmoja wa Yanga SC na wapinzani wetu, na soka tulilocheza kwenye mchezo
wa mwishoni mwa wiki kwa kweli ni dhahiri mwalimu amefikia mwisho
kimbinu na hana njia mbadala.
Young Africans SC imekua ikicheza
chini ya kiwango katika michezo ya Ligi Kuu hali iliyoplekea kupata
ushindi kwa tabu na wakati mwingine timu kupoteza pointi.
Ikiwa Brandts ataondoka mapema timu
itaendelea na mazoezi kama kawaida katika kila siku asubuhi katika
uwanja wa bora kijitonyama kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na
mashindano ya kimataifa chini ya kocha msaidizi Fred Felix "Minziro".
Ili kuhakikisha timu inafanya vizuri
katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom na mashindano ya
kimataifa uongozi unakamilisha maandalizi ya safari ya kambi nje ya nchi
na taratibu zote zitakapokamilika tutawajulisha.
Aidha uongozi upo katika mchakato wa
kumapata mrithi wa Brandts ambaye ataungana na timu kwa ajili ya
maandalizi ya mzunguko wa pili na Mashindano ya klabu Bingwa Afrika.
Mwisho tunawaomba wanachama, wapenzi
na washabiki wa Yanga wasivunjike moyo kufuatia matokeo ya bonanza
mwishoni mwa wiki, uongozi unajipanga kuhakikisha timu inaimarika kwenye
benchi la ufundi na kurudisha furaha katika mzunguko wa pili wa VPL.
Abdallah Bin Kleb
Mwenyekiti - Kamati ya Mashindano
Young Africans Sports Club.
DAR ES SALAAM
23 Disemba, 2013
No comments:
Post a Comment