Watu wawili ambao ni askari mgambo, wamekimbilia kusikojulikana bado,
wanatafutwa na polisi baada ya kumpiga kwa fimbo kichwani na kumwua mkulima
aliyetambulika kwa jina la Gigwa Malegi (55, Msukuma) na mkazi wa kijiji cha
Iyonyo.
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya,
Kamishna Msaidizi wa Polisi, Barakael Masaki inasema kuwa mauaji hayo yalitokea
tarehe Mosi Julai, 2013 majira ya saa moja jioni katika kijiji cha Totowe
wilayani Chunya, Mbeya.
Taarifa
hiyo imewataja watuhumiwa kuwa ni Focus Fabian na Charles (jina la pili
halijafahamika bado).
Imeelezwa kuwa chanzo cha kupigwa na kuuawa
marehemu kinatokana na kukutwa akilisha mifugo (ng'ombe) kaitka eneo oevu
kandoni mwa ziwa Rukwa.
Kamanda Masaki ametoa wito kwa jamii kuacha tabia
ya kujichukulia sheria mkononi badala yake amewasihi watatue matatizo yao kwa
mazungumzo na kwa kufuata sheria.
Ametoa wito kwa watuhumiwa
kujisalimisha mikononi mwa askari mara moja ama yeyote mwenye taarifa za
watuhumiwa, azitoe mara moja katika mamlaka husika ili hatua za kisheria
zichukuliwe.
No comments:
Post a Comment