VITA ya kupambana na utendaji kazi usiokuwa na tija kwa Taifa kwa watendaji wengi wa taasisi za Serikali imezidi kushika kasi baada ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, kumtaka Katibu wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk. Charles Msonde kumwandikia maelezo ya kitaalamu yaliyosababisha kubadilishwa kwa mfumo wa upangaji viwango vya ufaulu kutoka wa madaraja (Division) hadi wastani wa pointi (GPA).
Pia amemtaka kumweleza sababu zilizowafanya kuongeza mtihani (Continuous Assesment) kwa wanafunzi wa kujitegemea ili ajiridhishe pamoja na viongozi wengine wa wizara iwapo mabadiliko hayo yana tija kwa Taifa au la.
Profesa Ndalichako alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza kwenye kikao cha menejimenti ya baraza hilo.