Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa akizungumza kwenye mkutano na
waandishi Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema,
Tundu Lissu na Makamu Mwenyekiti (Zanzibar), Said Issa Mohamed.
Kamati Kuu ya Chadema imeazimia
kuendesha kampeni ya kupinga Katiba Inayopendekezwa kwa viongozi wake
wakuu pamoja na wale wa mabaraza yake kufanya ziara katika mikoa
mbalimbali nchini.
Hatua hiyo imekuja siku tatu, tangu Rais Kikwete
autangazie umma wa Watanzania alipokuwa akihutubia kilele cha Mbio za
Mwenge mkoani Tabora kwamba Katiba Inayopendekezwa inafaa hivyo kuwataka
Watanzania waipigie kura wakati wa mchakato wa kura ya maoni.
Ziara ya Chadema itaanzia katika mikoa ya Kanda ya
Ziwa ambako itachukua siku 20 ikiongozwa na Baraza la Wanawake
(Bawacha), linaloongozwa na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na baada ya
kumaliza, itaanza ziara nyingine ya siku 20 itakayofanywa na Baraza la
Vijana (Bavicha).
Dk Slaa alisema CCM wameanza kazi ya kuwataka
wananchi kupiga kura ya ‘ndiyo’ na Chadema wanaanza mikutano ya
kuwashawishi wananchi kuikataa kwa kuipigia kura ya ‘hapana’.
Alisema kuanzia Novemba 5 mwaka huu, viongozi wa ngazi za juu wa chama hicho nao wataanza ziara katika mikoa mbalimbali nchini.
“Bawacha ndiyo itakuwa timu ya kwanza. Itakwenda
Mwanza mjini, Ukerewe, Magu, Sengerema, Geita, Busanda, Bukombe,
Biharamulo, Muleba, Karagwe, Bukoba Mjini, Chato, Shinyanga Mjini na
Maswa Mashariki,” alisema Dk Slaa. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz