Thursday, May 18, 2017

MWILI WA MTOTO ALIEPOTEA, WAKUTWA HAUNA MACHO, ULIMI NA MENO MAWILI

Mtoto Felister Isack Skali (7) pichani, ambaye alikuwa mwanafunzi wa chekechea katika Shule ya msingi Mwagala Mbuyuni Wilaya ya Songwe Mkoa wa Songwe aliyetoweka katika mazingira ya kutatanisha tangu mei 11 mwaka huu, mwili wake umekutwa porini ukiwa hauna baadhi ya viungo kama ulimi, macho na meno mawili ya chini.

Akithibitisha kupatikana kwa mwili wa marehemu Afisa Mtendaji wa kijiji cha Mbuyuni Athanas Hamis amesema alipata taarifa kutoka kwa wachungaji wa mifugo ambapo alifika eneo la tukio jioni na wanachi kulazimika kulinda mwili hadi asubuhi walipofika askari Polisi wa kituo cha Galula na Daktari na kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu kisha mazishi kufanyika jana.

Tukio hilo ni la kwanza kutokea katika kijiji cha Mbuyuni ambalo linahusishwa na imani za kishirikina.

Friday, May 05, 2017

UPELELEZI ALIYEJITOSA BAHARINI WAKAMILIKA

Wakati Polisi Zanzibar ikisema imekamilisha kumhoji msichana aliyejitosa Bahari ya Hindi eneo la Chumbe alipokuwa akisafiri na boti ya Kilimanjaro (V) kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar, mtaalamu anasema binti huyo amethirika kisaikolojia ni bora angeachwa apumzike.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Hassan Nassir Ali alimwambia wa habari hii jana kuwa, msichana huyo anayesoma kidato cha tatu Sekondari ya Glorious na watu wengine wameshahojiwa kuhusu tukio hilo la Aprili 3.

Hassan alisema miongoni mwa walihojiwa ni wanafamilia, msichana huyo na manahodha wa boti ya Kilimanjaro ambao walimuokoa.

Alisema polisi imepata taarifa kamili juu ya tukio hilo, hivyo wakati wowote jalada litafikishwa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa hatua zaidi za kisheria.

PENGO APELEKWA MAREKANI KWA MATIBABU

ASKOFU wa Kanisa Katoliki  Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amepelekwa nchini Marekani kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya yake.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari, Dar es Salaam jana na Askofu Msaidizi wa jimbo hilo, Eusebius Nzigilwa alisema Kardinali Pengo alisafirishwa Mei 2, mwaka huu kwa ajili ya kupatiwa matibabu na kufanyiwa uchunguzi.

Alisema Kardinali Pengo, anatarajiwa kuwapo nchini Marekani kwa mwezi mmoja.

“Tuendelee kumuombea Baba Kardinali Pengo ili mwenyezi Mungu amjalie nguvu na afya njema ya mwili na roho ili aweze kuliongoza vema Taifa la Mungu alilokabidhiwa,”alisema  Nzigilwa.

Hivi karibuni, hali ya afya ya Kardinali Pengo, ilionekana kudhoofu kutokana na maradhi yanayomsumbua, kitendo kilichosababisha ashindwe kuongoza misa za ibada kanisani.

Wakati wa misa ya Sikukuu ya Pasaka iliyofanyika hivi karibuni, Kardinali Pengo alionekana kudhoofu na kufikia uamuzi wa kukataa kupigwa picha na waandishi wa habari waliohudhuria misa hiyo.

Thursday, April 20, 2017

TFDA YAPOKEA MAOMBI 767 YA VIWANDA VIPYA

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Chakula na Dawa(TDFA), Hiiti Sillo amesema kuanzia Machi mwaka huu taasisi yake ilimepokea maombi mapya ya usajili wa viwanda 767.

Amesema katika maombi hayo, viwanda 635 vipya vimesajiliwa kati ya hivyo, 613 vya chakula, kimoja cha dawa na 21 vya vipodozi akisema hiyo ni asilimia 82.8 ya maombi yote jambo linaloashiria kwamba waombaji wengi wanazingatia sheria.

Amesema katika kipindi hicho TFDA ilifanya tathmini ya maombi 4,762 sawa na asilimia 82.1 ya usajili wa bidhaa za dawa, chakula, vifaatiba na vipodozi, kati ya maombi 5,802 yaliyowasilishwa na 4,322 (75%) yaliidhinishwa na 440 yalikataliwa kwa kutokidhi vigezo vya ubora.

Sillo ameeleza hayo leo kwenye mkutano na wahariri wa vyombo vya habari walipokutana mkoani Tabora.

'UPINZANI HAUNINYIMI USINGIZI' MUGABE

Viongozi wawili wa vyama vya upinzani nchini Zimbabwe wamekubaliana kuunda umoja kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu ujao nchini humo.

Kiongozi wa Movement for Democratic, Morgan Tsvangirai na aliyekuwa makamu wa rais wa nchi hiyo Joice Mujuru wa National people's Party walitia saini makubaliano hayo siku ya Jumatano.

Rais wa nchi hiyo Robert Mugabe awali alitoa maneno ya dhihaka kutokana na mipango ya upinzani aliyodai kuungana kumuondoa madarakani.
Morgan Tsvangirai na Joice Mujuru wameonekana kumaliza baadhi ya tofauti zao.Tsvangirai anasema makubaliano yaliyotiwa saini baina ya vyama viwili ni msingi kuelekea kuunda umoja wa vyama kwa ajili ya kupambana na chama tawala Zanu PF.

Changamoto iliyopo hivi sasa ni kuamua nani kati ya hao wawili ataongoza muungano huo.

Tayari, vyama vingi vidogo vya upinzani vimemuidhinisha Morgan Tsvangirai kuwa mgombea wao wa urais.

Kiongozi wa miaka mingi madarakani Robert Mugabe , alieleza kuwa upinzani umejaa watu wasio na kitu vichwani.

Amesema hakosi usingizi kwa kile kinachoitwa umoja wa wapinzani.

MADAKTARI 258 WALIOKUWA WAKAAJIRIWE KENYA, SASA KUAJIRIWA NCHINI

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu

Madaktari 258 ambao walikidhi vigezo vya kwenda kufanya kazi nchini Kenya, sasa wataajiriwa na serikali ya Tanzania kutokana na kuwepo na zuio la Mahakama ya Kenya la kuwaajiri.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya Rais Magufuli kumwelekeza jana kuwa awaajiri madaktari hao pamoja na wataalam wengine wa afya 11.

Madakatari hao walioomba hizo nafasi za kwenda Kenya walikuwa 496 kati ya 500 waliotakiwa, 258 ndio wakakidhi vigezo.

Mkataba wa Tanzania na Kenya ilikuwa mpaka Aprili 6 wawe wamepatikana hao madaktari na kati ya Aprili 6 mpaka 10 wasafirishwe kwenda Kenya, sasa baada ya kuajiriwa na serikali, Kenya wakiwa tayari na kuhitaji tena madaktari  watatafutiwa wengine.

Sunday, April 16, 2017

MABWENI MAPYA YA UDSM KUHUDUMIA WANAFUNZI 3840

Mabweni mapya ya wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yana uwezo wa kuchukua jumla ya wanafunzi 3,840 kwa uwiano wa wanafunzi 192 kwa kila jengo.

Akizungumza leo wakati Rais John Magufuli akizindua mabweni hayo, Makamu Mkuu  wa Chuo hicho, Profesa  Rwekaza Mukandala, mabweni hayo ni mjumuiko wa majengo 20 yenye ghorofa nne kila moja na vyumba 12 kwa kila ghorofa.

Profesa Mukandala amemwambia Rais  Magufuli kuwa chuo chake kimechangia ujenzi wa mabweni hayo kwa kutengeneza vitanda 1920, makabati 1920, droo 1920, meza 1920, viti 3,840 na magodoro 3,840.

JAMBO TZ TUNAWATAKIA PASAKA NJEMA WAKRISTO WOTE.



Monday, March 27, 2017

WIMBO WA NAY WA MITEGO SASA RUKSA

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Harrison Mwakyembe, ameondoa zuio la kufungiwa kwa wimbo wa ‘Wapo’ wa mwanamuziki Nay wa Mitego.

Akizungumza na waandishi mjini Dodoma leo, Waziri Mwakyembe alimtaka mwanamuziki huyo auboreshe wimbo huo na ikiwezekana aende Dodoma ili akamuongezee maneno zaidi.

Kabla ya kauli ya Dk Mwakyembe ya kuondoa zuio hilo, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) lilizuia kupigwa au kusikilizwa kwa wimbo huo.

 Jana msanii huyo alikamatwa akiwa Morogoro katika shughuli zake za muziki na kuletwa jijini Dar es Salaam, kwa kile kilichoelezwa kuwa wimbo wake umeikashfu serikali.

RIPOTI: FARU JOHN ALIKUFA KWA KUKOSA UANGALIZI WA KARIBU.

Faru maarufu kwa jina John, ambaye alikufa mwaka jana, alikufa akiwa katika hifadhi ya Sasakwa Grumeti kwa kukosa matunzo na uangalizi wa karibu, ripoti ya uchunguzi inasema.

Uchunguzi huo ulioongozwa na Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. Samwel Manyele uligundua kuwa kulikuwa na mapungufu katika kumtunza mnyama huyo kabla ya kufa kwake Prof Manyele amesema miongoni mwa mengine, hakukuwepo na kibali rasmi cha kumhamisha Faru John.
Aidha, hakukuwa na mkataba wa kupokelewa kwa Faru John hifadhi ya Sasakwa Grumeti na afya na maendeleo ya Faru John baada ya kuhamishwa haikufuatiliwa. Prof Manyele alisema hayo alipowasilisha ripoti ya uchunguzi kwa Waziri Mkuu wa Kassim Majaliwa.

"Sababu za kifo chake zilichangiwa na kukosa matunzo na uangalizi wa karibu, kukosa matibabu alipoumwa, mazoea yanayotokana na kutofuata taratibu zilizowekwa kisheria na mapungufu ya kiuongozu kwa Wizara husika, hifadhi na taasisi zake," alisema.

Sunday, March 26, 2017

TANESCO YAIDAI JWTZ BILLION 3.

Mkuu wa Majeshi nchini, Evance Mabeyo amesema Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) linadaiwa Sh3 bilioni na Shirika la Umeme nchini na kesho (Jumatatu)  watapunguza deni hilo ili wasikatiwe umeme.

Mabeyo ameyasema hayo leo wakati anazungumza na waandishi wa habari makao makuu ya jeshi (Ngome) na kueleza deni hilo limetokana na shughuli za jeshi hilo kwenye ulinzi wa Taifa pamoja na ufinyu wa bajeti.

"Baada ya kupokea maelezo ya TANESCO na kufuatia tamko la Rais, Jeshi la Wananchi limetafakari na limefanya jitihada kupata fedha za  kupunguza deni hili, tunadaiwa fedha kiasi kinachozi kidogo Sh3 bilioni, nimeagiza watendaji wetu watafute Sh1 bilioni," amesema Mabeyo.

Mabeyo amesema juhudi zinazofanywa na Jeshi hilo zinatakiwa kuonyeshwa na Taasisi nyingine ili kuweza kuiongezea TANESCO uwezo wa kutoa huduma.

Friday, March 24, 2017

MWIGULU AAGIZA ASKARI ALIEMTISHA NAPE KWA BASTOLA AKAMATWE....!!!

Waziri wa mambo ya ndani Mwigulu Nchemba ameshutumu kitendo cha askari mmoja kuchomoa bastola na kumtisha Nape Nnauye wakati maafisa hao wa usalama walipokuwa wanajaribu kumzuia aliyekuwa waziri wa habari kuhutubia wanahabari.

Mwigulu, kwenye ukurasa wake wa Facebook, amesema kitendo hicho si cha busara na kwamba afisa mhusika kuadhibiwa.

Amesema amemwagiza mkuu wa jeshi la polisi kutumia picha zilizopigwa wakati wa tukio hilo kumska mhusika.

 "Nape Moses Nnauye sio jambazi, ni mtanzania, ni mbunge, mjumbe wa NEC wa CCM, hana record ya uhalifu. Kitendo cha mtu kumtolea bastola, sio cha kiaskari, sio cha kitanzania na sio cha ki Mungu, kama mtu ameweza kutoa bastola mbele ya kamera nawaza mbali ingekuwa kwenye uchochoro angefanya nini," ameandika.

"Nahusika na usalama wa raia wote wa Tanzania, nimemwelekeza IGP atumie picha kumsaka mtu yule aliyeinua kufanya kitu cha kihalifu kwa kofia ya uaskari. Na kama ni askari basi sheria zinazoongoza taasisi husika zichukue mkondo wake.

Sunday, March 19, 2017

ZANZIBAR YAANZA KULIPA DENI LA UMEME

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imeanza kulipa deni lake inalodaiwa na shirika la umeme Tanzania (TANESCO).

Taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa imesema kuwa Profesa Muhongo amesema SMZ imelipa kiasi cha Sh10 bilioni na itaendelea kulipa deni hilo hadi litakapomalizika.

Tuesday, March 14, 2017

WANANCHI WAANDAMANA NA JENEZA HADI KWA DIWANI, WATAKA KUZIKA OFISI KWAKE.

Wananchi wa Kata ya Mhongolo mjini Kahama jana waliandamana wakiwa na  jeneza la mtoto aliyefariki mtaani hapo kwa lengo la kwenda kuuzika mwili huo kwenye Ofisi ya kata hiyo wakidai diwani wa kata hiyo, Michael Mizubo ameuza eneo la makaburi kwa maslahi yake binafsi.

Mmoja wa wananchi hao aliyejulikana kwa jina moja la Paulina ambaye alikuwa akiongoza maandamano hayo, amesema waliamua kwenda kuzika mwili huo wa mtoto huyo aliyejulikana kwa jina moja la Rosemary aliyefariki kwa ugojwa wa kawaida kwenye ofisi hiyo ya kata, kwa sababu hakuna eneo la kuzika.

Hata hivyo wakati wanachimba kaburi hilo kwenye mlango wa ofisi ya diwani huyo kwa lengo la kuuzika mwili huo polisi walifika na kuwatawanya kwenye eneo hilo kwa madai ni ukiukwaji wa taratibu.

Kwa upande wake diwani wa kata hiyo Mizubo anayedaiwa kuuza eneo la maziko amesema  wananchi hao walikuwa na sababu zao za kisiasa kwani pamoja na eneo hilo la makaburi kuuzwa tayari kuna eneo jingine limetengwa kwa ajili ya maziko hayo.

Chanzo: Gazeti la Mwananchi.

TRUMP HAJUI APELEKE WAPI DOLA 400,000 ZA MSHAHARA WAKE

Rais wa Marekani Donald Trump

Msemaji wa ikulu ya White House amesema Rais Donald Trump atatoa mshahara wake kama hisani kwa mashirika yanayosaidia wasiojiweza katika jamii.

Sean Spicer amesema anataka waadhishi wa habari wanaoripoti taarifa kuhusu White House na Rais wa Marekani wamsaidie kuchagua nani wanafaa kupewa pesa hizo.

Mshahara wa Bw Trump utakuwa umefikia dola 400,000 kufikia mwisho wa mwaka.

Wakati wa kampeni za urais, Bw Trump alisema kwamba hakupanga kupokea mshahara wake na kwamba badala yake angepokea dola moja pekee ambayo ni lazima kisheria.

Alikosolewa wakati wa kampeni baada ya taarifa kuibuka kwamba alikuwa ametoa kiwango kidogo sana cha pesa kama hisani licha ya utajiri wake mkubwa.

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...