Mwaka wa
uchaguzi umeingia. Usiku wa kuamkia leo, Watanzania wameupokea mwaka
mpya 2015 huku tafakari kubwa ikiwa ni matukio makubwa yatakayotokea
mwaka huu, ukiwamo Uchaguzi Mkuu na kura ya maoni ya Katiba
Inayopendekezwa.
Mbali na uchaguzi wa rais wa awamu ya tano,
wananchi wataamua ama kuipitisha au kuikataa Katiba Inayopendekezwa,
mambo ambayo wasomi, wanasiasa na wanaharakati wameonya kuwa yanatakiwa
kuendeshwa na kusimamiwa kwa weledi na umakini mkubwa.
Vilevile, kutokana na matukio hayo kugharimu fedha
nyingi, wataalamu wa uchumi wanatabiri kuwa mwaka huu utakuwa mgumu na
itakaowalazimu Watanzania kufunga mikanda zaidi.
Pia, macho na masikio ya wananchi yako kwa vyama
vya upinzani ambavyo vimeungana na kuzaa Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) kuona kama vitasimamisha mgombea mmoja wa urais na katika nafasi
za ubunge na udiwani kama vilivyokubaliana, ikiwa ni mara ya kwanza
tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.