Uongozi wa Yanga umepanga
kuliandikia Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) kuishtaki TFF kwa
kukiuka Kanuni ya 19 ya usajili katika kufanya uamuzi wa utata wa
usajili wa mshambuliaji wa Uganda, Emmanuel Okwi.
Kikao cha Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji
ya TFF kilichofanyika jijini Dar es salaam juzi, kiliamua kumtangaza
Okwi kuwa mchezaji huru baada ya kubaini kuwa Yanga ilivunja mkataba kwa
kutomlipa stahiki zake za usajili na pia kuandika barua TFF kutaka
mkataba wake na Mganda huyo uvunjwe, uamuzi ambao umeinufaisha Simba
ambayo imemsajili.
Mkataba wa mchezaji huyo ulipitiwa na kamati hiyo
ikiwamo kumsikiliza mchezaji mwenyewe pamoja na Yanga na kuridhika kuwa
mkataba kati ya pande hizo umevunjika.
Kamati hiyo ilisema ukiwa ni mkataba wa pande
mbili, Yanga ilikiuka kipengele namba nane kuhusu malipo ya ada ya
usajili. Yanga ikiwa mwajiri, haikutekeleza kipengele hicho hadi kufikia
Juni 27 mwaka huu, ilipoandika barua TFF kuomba mkataba huo uvunjwe.
Kwa maana hiyo Okwi ni mchezaji huru, hivyo yuko huru kujiunga na timu
yoyote.
Hata hivyo, uongozi wa Yanga jana ulisema
haukubaliani na uamuzi huo na kwamba walikuwa wameshaandika barua
kupinga baadhi ya wajumbe katika kamati ya sheria ya TFF wasisikilize
kesi yao, akiwamo mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia
Hans Pope ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo ya sheria.