MWANAFUNZI wa darasa la saba katika Shule ya Msingi ya Sokoine, Manispaa ya Dodoma (jina linahifadhiwa), anadaiwa kuwekwa kinyumba na mwalimu wake David Macha (30).
Mwanafunzi huyo wa miaka 14 ni kati ya watoto wanaofadhiliwa na shirika lisilo la kiserikali la Compassion International Tanzania kituo cha Tz 807 FPCT kilichoko Chamwino.
Hata hivyo, katika hali ya kushangaza Jeshi la Polisi mkoani hapa, limelalamikiwa na wazazi wa mtoto huyo kwa kitendo cha kumlinda mtuhumiwa licha ya kupewa taarifa za uhalifu huo kwa zaidi ya miezi mitano sasa, limeshindwa kumchukulia hatua.
Uchunguzi wa Tanzania Daima ambao umethibitishwa na wazazi wa mwanafunzi huyo, umebaini kuwa mwalimu Macha amekuwa akifanya mapenzi na mwanafunzi huyo kwa zaidi ya miezi mitano sasa.
Wazazi wa mwanafunzi huyo wanathibitisha kuwa kwa zaidi ya miezi mitano, mtoto wao alikuwa na tabia ya kutoroka nyumbani nyakati za usiku na kulala nje, jambo ambalo lilianza kuwatia mashaka na kuanza kufuatilia nyendo zake.
Walidai kuwa wakati mwingine alikuwa akirudi nyumbani asubuhi kwa ajili ya kujiandaa kwenda shule na anapoulizwa alikolala, alisema alikuwa katika mkesha.
Akisimulia mkasa huo, mjomba wa mwanafunzi huyo, Silas Mjengi, alisema binti yao anaishi na mama yake pekee katika eneo la Area ‘A’ mjini hapa baada ya mzazi huyo kutengana na mumewe.