Bismillar Rahmanir Rahiim
JUMUIYA NA TAASISI ZA KIISLAM (T)
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI JUU YA KUCHUKULIWA NA POLISI SHEIKH PONDA ISSA PONDA TOKA HOSPITALI
Jana asubuhi majira ya saa nne na nusu askari wa jeshi la Polisi na watu wanaoaminika kuwa usalama wa taifa walikwenda hospitali ya Muhimbili (MOI) na kumchukua Sheikh Ponda Issa Ponda. Juhudi za Sheikh Mwenyewe, mkewe na waislam waliokuwepo pale hospitali kutaka abaki hospitalini kuendelea na matibabu hazikuzaa matunda. Mpaka Sasa bado tunafuatilia kujua mahali Kiongozi huyo wa Kiislam alikopelekwa.
Tumepokea kwa masikitiko makubwa sana habari hizi na tunashindwa kuamini kama mambo haya yanaweza kufanywa na Serikali inayodai kutawala kwa kufuata utawala bora unaojali sheria, uadilifu, utu na uhuru wa kujieleza.
Kitendo cha kumpiga risasi Sheikh Ponda na kisha kumchukua toka hospitalini na kumpeleka Gerezani kwa kukiuka taratibu ni kinyume cha haki za binadamu, utawala bora na uhuru wa maisha ya mtu. Matibabu ni haki mojawapo kwa binadamu yoyote hata kama kuna wanaomtuhumu. Tuhuma juu ya mtu si sababu ya kukiuka taratibu, kuvunja sheria na hata kumtisha unayemtuhumu kwani njia hiyo haiwezi kutatua tatizo bali inalifanya kuwa kubwa zaidi.