MKURUGENZI wa Mashitaka nchini (DPP), Dk. Eliezer Feleshi, amefuta kesi ya kuteka na kujaribu kumuua Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, iliyokuwa ikimkabili raia wa Kenya, Joshua Mulundi, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni baada ya DPP kuona hana haja ya kuendelea kumshitaki kwa makosa hayo ambayo yalikuwa hayana dhamana.
Hati hiyo ya DPP iliwasilishwa chini ya kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 kwa niaba yake na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka, jana mbele ya Hakimu Mkazi Waliarwande Lema.
Kweka aliiambia mahakama kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa lakini upande wa Jamhuri hauna nia tena ya kuendelea kumshitaki Mulundi kwa kesi hiyo.
Hakimu Lema alikubaliana na hoja hiyo na akamfutia kesi hiyo Mulundi ambaye yupo gerezani tangu Julai 13, mwaka jana.