Muda wa saa 48 wa kusalimisha silaha kwa waasi wa March 23(M23), Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umemalizika na wakati wowote mapigano yanaweza kuanza.
Misheni ya Kutuliza Amani ya Umoja wa Mataifa(Monusco) , ilitoa saa hizo zinazomalizika leo na Jeshi la UN litaanza kutumia nguvu kunyang’anya silaha waasi hao.
Taarifa ya Monusco iliyotolewa na Msimamizi wa Misheni hiyo, Luteni Jenerali Carlos Alberto dos Santos Cruz na kusambazwa na Idara ya Mawasiliano ya Umoja wa Mataifa jana, inaeleza kwamba, watu binafsi katika eneo la Kivu ya Magharibi ambalo linajumisha Goma na Sake na ambao hawahusiki na vyombo vya usalama wamepewa saa 48 kuanzia saa kumi jana (juzi) kwa saa za Goma (Jumanne) kuzisalimisha silaha zao.
Taarifa ilisema, “Baada ya saa 10 jioni ya Alhamisi,
Agosti Mosi, wale wote ambao watakuwa hawajasalimisha silaha zao watachukuliwa
kama tishio kwa usalama wa wananchi na Monusco itachukua hatua zote muhimu
kuwapokonya silaha hizo ikiwa ni pamoja na kutumia nguvu kama ilivyoainishwa
katika mamlaka na sheria za ushiriki za Monusco.”