Rais
Kikwete akitoa heshima za mwisho kwa marehemu askari waliouwawa huko
Darfur wakitekeleza majukumu ya umoja wa mataifa ya kulinda amani.
Dar es Salaam.
Rais
Jakaya Kikwete ameutaka Umoja wa Mataifa (UN), kuruhusu kutumika kwa
mtutu katika operesheni za kulinda amani zinazoendelea.
Alitoa
kauli hiyo jana baada ya kutoa heshima zake kwa wapiganaji saba wa
Tanzania waliokuwa Darfur, Sudan katika operesheni ya kulinda amani ya
UN na Afrika (Unamid) ambao waliuawa na kundi linalodaiwa la wanamgambo
wa Janjaweed wanaoungwa mkono na Serikali ya Sudan inayoongozwa na Rais
Omar al-Bashir.
Wapiganaji waliouawa ni Oswald Chaula kutoka 42KJ
Chabruma, Songea, Peter Werema (44KJ Mbeya), Fortunatus Msofe (36KJ
Msangani, Pwani), Rodney Ndunguru (92KJ Ngerengere), Mohamed Juma (94KJ
Mwenge), Mohamed Chukilizo (41KJ Nachingwea) na Shaibu Othman (MMJ-
Upanga).
“Lazima nikiri kuwa taarifa hiyo ya vifo vya vijana wetu
ilinihuzunisha, kunisikitisha na kunikasirisha. Kwa nini watu wa Darfur
wawaue wanajeshi wetu ambao wamekwenda kule kuwasaidia wapate utulivu
ili kunusuru maisha yao, kuwaondolea wasiwasi na kuwawezesha wafanye
shughuli zenye tija kuendesha maisha yao?
“Moja kwa moja sikusita
kuamini kuwa waliofanya hivyo ni watu wahalifu. Tangu uhuru ni sera ya
nchi yetu kutetea wanyonge dhidi ya ukoloni, ubaguzi, uonevu, dhuluma na
watu wote walioko katika mazingira hatarishi Afrika na duniani. UN
ifanyie marekebisho sheria ili majeshi yanayolinda amani yawe na nguvu
za kujihami ili kuzuia maafa yanayoweza kujitokeza.”