
KUPINGA KAULI YA WAZIRI MKUU "Wapigwe tu" ALIYOITOA BUNGENI TAREHE 20/06/2013
Taarifa hii ni matokeo ya ufuatiliaji wa utendaji wa shughuli za Serikali kama zinavyowasilishwa bungeni na kauli ya Waziri Mkuu (Mtendaji Mkuu wa shughuli za serikali Bungeni) aliyoitoa, Alhamisi ya tarehe 20 Juni 2013, wakati akijibu maswali ya papo kwa hapo. Waziri Mkuu Pinda, alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama, hususan Jeshi la Polisi kuwapiga wananchi watakao kaidi na kupinga amri halali ya jeshi hilo. Katika tamko hilo, Pinda alisema Serikali imechoshwa na vurugu na kwamba hakuna namna nyingine ya kupambana na wananchi wanaodharau vyombo vya dola zaidi ya kipigo.
Waziri Mkuu Pinda alitoa msimamo huo Bungeni, wakati akijibu swali la Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM), aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa na Serikali kufuatia kuwa na matukio ya vurugu ya mara kwa mara nchini, hususan huko Mtwara na Arusha.
Katika majibu yake, Mh. Pinda, pamoja na mambo mengine alisema kuwa; “Mheshimiwa Mangungu hapa ameanza vizuri, lakini mwisho hapa naona anasema vyombo vya dola vinapiga watu, ukifanya fujo au umeambiwa usifanye hiki ukaamua kukaidi utapigwa tu. Akaendelea kusema kuwa, “Lazima wote tukubaliane kuwa nchi hii tunaiendesha kwa misingi ya sheria na kama wewe umekaidi, unaona kwamba ni imara zaidi, wewe ndio jeuri zaidi, watakupiga tu.