Na Mwandishi Wetu
MWILI
wa mwanamuziki Langa Kileo jana (Jumatatu) ulipumzishwa kwenye nyumba
ya milele katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar lakini nyuma ya kifo
chake kuna siri ambayo rafiki yake wa karibu (jina linahifadhiwa) mkazi
wa Mikocheni A jijini Dar ameamua kuiweka hadharani.
Akizungumza
na Uwazi juzi, rafiki huyo wa marehemu alisema, siku chache kabla ya
kifo chake alimfuata na kumwambia kuwa Israel mtoa roho anamtembelea
usiku na anahisi siku si nyingi atamfuata mshikaji wake aliyetangulia
mbele ya haki, Albert Mangweha ‘Ngwea’.
“Hii
ni siri ambayo hata ndugu zake hawaijui lakini mshikaji alijua anakufa.
Alijitahidi kukikwepa kifo lakini alishindwa. Siku chache kabla hajafa,
usiku alikuja kwangu na kuniambia kule kwao kwenye geto lake analoishi
ambalo liko ghorofani, anaona mauzauza na anahisi kifo kinamuita.
“Nilishangazwa
sana na maneno yale. Akazidi kuniambia eti kwa jinsi mambo
yanavyokwenda hawezi kuendelea kulala kwao na kuanzia siku ile angelala
na mshikaji wetu mwingine pale Geza, Mikocheni A.
“Kweli
siku hiyo alilala pale akiwa na hofu kubwa na asubuhi baadhi ya watu
wakawa wanamshangaa akiwa ‘amezima’ nje ya lile geto la mshikaji wake.
Alivyoondoka sikumuona tena mpaka nilipokuja kuambiwa yuko hoi kwa
malaria na kesho yake nikasikia hatunaye, nimeumia sana,” alisema mtoa
habari huyo.
Alipoulizwa juu ya
uhusiano wa kifo cha Langa na matumizi ya madawa ya kulevya, rafiki huyo
alisema: “Inaweza ikawa ngumu kwa ndugu wa marehemu kuhusisha kifo
chake na madawa ya kulevya lakini mimi namjua Langa nje ndani, ukweli ni
kwamba jamaa alikuwa akiendelea kula ‘mambo’.
“Alikuwa
anakuja maskani tunakula mambo yetu na hata wakati anafanya kazi kwenye
ile Kampuni ya Barrick hapa Dar, ilikuwa kabla hajaenda anapita kwanza
huku uswahilini kisha ndiyo anaenda. Kwa maana hiyo malaria ndiyo
iliyomuua lakini hata madawa yamechangia.”
Langa
alifariki dunia Juni 13, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili
jijini Dar. Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi. Amini!
SORCE: Globalpublishers