Wakati
Jeshi la Polisi nchini limesema limepata taarifa za mwonekano wa mtu
aliyetupa bomu katika mkutano wa kampeni wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) Arusha,Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe
amesema wabunge wake leo hawataingia bungeni.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Mbowe alisema wabunge hao watawasili
Arusha kwa ajili ya kuungana na wananchi pamoja na wanachama kwenye
msiba huo.
Alisisitiza
kwamba kuanzia leo mahema yatawekwa viwanja vya Soweto kwa ajili ya
kuomboleza msiba huo na mara polisi wakimaliza uchunguzi wao na kutoa
majibu juu ya vifo hivyo, marehemu hao watasafirishwa.
Wakati
Mbowe anatoa kauli hiyo Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi
akizungumza jana mjini Arusha na waandishi wa habari, alisema taarifa za
awali zinaonesha mlipuko huo ni bomu la kutupwa kwa mkono (grumeti) na
hivi sasa timu ya wataalamu ikiongozwa na Kamishna wa Operesheni
Maalumu wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja inaendelea na uchunguzi wa
tukio hilo.
Naye
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP),
Said Mwema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari ameahidi kupambana
na kuhakikisha wahusika wanapatikana.