Rais wa Ufaransa, Francois Hollande, ametia saini sheria yenye utatanishi, inayohalalisha ndoa kati ya watu wa jinsia moja.
Ufaransa sasa imekuwa nchi ya 14 duniani kuruhusu ndoa kama hizo.
Makundi ya watu wanaofanya mapenzi ya jinsia moja nchini Ufaransa yamefurahi kuwa hatimaye sheria hiyo imepitishwa.
Wanasema kuna marafiki kadha wanaosubiri kufunga ndoa na maelfu ya watoto wanaolelewa na watu wa jinsia moja
ambao sasa watapata hifadhi kisheria.
Wanaopinga sheria hiyo wamehamaki.
Wanaona kuwa Rais Hollande ameshughulika mno na ndoa kati ya jinsia moja kwa sababu ameshindwa katika maswala muhimu zaidi - kama swala la uchumi wa nchi.
Maandamano mengine ya kupinga ndoa kati ya jinsia moja yanapangwa kufanywa tarehe 26 May.
Yanaweza kuwa makubwa na ya fujo kama yaliyopita.
Sababu ni upinzani dhidi ya ndoa za jinsia moja umechanganyika na malalamiko mengine ya mrengo wa kulia dhidi ya serikali.
Na hali nchini sasa ni tete.
Lakini kwa kweli vita vimemalizika.
Watu wa jinsia moja sasa wataanza kufunga ndoa nchini Ufaransa.
Baadhi ya wanasiasa wa mrengo wa kulia wataahidi kuwa watabatilisha sheria hiyo wakipata madaraka, lakini historia inaonesha kuwa kufuta mabadiliko kama haya katika jamii ni shida sana.