SKENDO nzito inalitafuna Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikitawala madai kwamba kuna wabunge wawili wanawake, wamejazwa mimba na waheshimiwa wenzao wanaume.
Awali, ulitawala uvumi kuwa mmoja wa wabunge wa upinzani (viti maalum), akitokea Kanda ya Kaskazini, amepewa ujauzito na mheshimiwa mwingine ambaye ni kiongozi anayeshika nafasi za juu kwenye moja ya vyama vikuu vya upinzani nchini (wote majina yao tunayahifadhi kwa sasa).
Kashfa hiyo ya mtunga sheria huyo kupewa mimba na mheshimiwa mwenzake ambaye ni mume wa mtu, ilipata mbeleko na kuifanya ivume zaidi, baada ya Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde (pichani), kulipuka bungeni: “Humuhumu ndani kuna wabunge wanawake wenye mimba zisizotarajiwa.”
Lusinde, alitamka hayo Aprili, mwaka huu, wakati akichangia hotuba ya bajeti, Ofisi ya Waziri Mkuu, kipindi ambacho bunge lilikuwa limechafuka kutokana na wabunge kurushiana ‘mipasho’ wao kwa wao.
Kauli ya Lusinde, pamoja na kupokelewa tofauti na wabunge wengi wanawake, wakidai mheshimiwa mwenzao amewadhalilisha, upande mwingine, katika ‘vikao vya kwenye korido’, matukio ya vicheko na kugonga mikono yalitawala na kunena kwa msisitizo “message delivered”, yaani ujumbe umefika.
Wakati mwandishi wetu akifuatilia sakata lenyewe, mbunge mwingine wa Viti Maalum (CCM) ambaye jina lake tunaliweka kabatini, aliamua kufunguka: “Nashangazwa sana na haya madai, tunawasema wapinzani, wakati hata kwetu (CCM) kuna watu wamepeana mimba.”