MIPANGO
endelevu inapaswa kufuatwa na kila mwanadamu, katika familia zetu za
Kiafrika mara nyingi tunaanguka katika suala la mipango mikakati ya muda
mrefu. Mwanadamu akifariki, mara nyingi wanaoachwa kuendeleza kazi za
marehemu wanaishia kusuasua na kutofikia malengo.
Yapata
mwaka mmoja tangu, aliyekuwa legend wa simema za Kibongo, Steven
Kanumba ‘The Great’ afariki dunia na kuiacha Kampuni yake ya Kanumba The
Great Film ikiendeleza shughuli zake za kuzalisha filamu kama kawaida.
Kampuni
aliyoiacha pale Sinza-Mori, jijini Dar ilibaki chini ya mikono ya
wafanyakazi wake wakiongozwa na mdogo wa marehemu, Seth Bosco, mpiga
picha za video, Zakayo Magulu pamoja na Mayasa Mrisho ‘Maya’ ambaye
alikuwa akifanya kazi kama msimamizi wa ‘location’ (location manager) na
masuala ya makeup.
Kadiri
siku zilivyozidi kusonga, umoja kati yao ulianza kupungua. Kila mmoja
anaonekana kuhangaika kivyake licha ya kwamba kampuni bado ipo. Mikakati
ya jumla ikawa haijadiliwi, kila mmoja akawa anaangalia namna ya
kujikwamua kivyake.
Mara
kadhaa nimekuwa nikizungumza na baadhi ya wasanii waliokuwa tegemezi
katika kampuni hiyo, wamekuwa wakiniambia wapo bize kufanya kazi zao
binafsi nje ya Kanumba The Great Film. Hiyo inaonesha dalili kwamba kazi
za umoja zimeanza kulegalega.
Marehemu Steven Kanumba akiwa na tuzo za filamu enzi za uhai wake.