NCHI ya Uruguay yenye raia takribani
milioni 4, inatajwa kuwa na bahati ya kuwa na Rais asiye na chembe ya
tamaa. Hana makuu, kiasi kwamba anatajwa kuwa ndiye Rais masikini zaidi
kuwahi kutokea duniani.
Huyu si mwingine, bali ni Jose Mujica,
Rais wa sasa wa Uruguay ambaye pia ni Rais wa 40 wa nchi hiyo. Tangu
aingie madarakani Machi mosi mwaka 2010, amekuwa akionekana kuwa
kiongozi wa tofauti kabisa, tofauti na waliomtangulia.
Mathalan, baada ya kufanikiwa kuishika
nchini, hakuwa na tamaa ya kukimbilia Ikulu, yeye alichokifanya ni
kuamua kuishi katika makazi yake yaleyale, katika nyumba ya mkewe
iliyoko shambani, nje ya Jiji la Montevideo.
Kwa ujumla, anapenda maisha ya kawaida, maisha ya kuwahurumia wengine na kujitahidi kuonesha kwa vitendo.
Ni vigumu kuamini, licha ya kuwa ni Rais
wa nchi, amejishusha mno kiasi cha mara kadhaa kuonekana akijichanganya
na raia wake katika shughuli za ujenzi wa taifa, ikiwamo ujenzi wa
barabara, kulima mashamba ya mfano.