Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini, Issaya
Mulungu, amesema upelelezi kuhusu tuhuma za vitendo vya ugaidi
zinazomkabili Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred
Lwakatale na mwenzake Joseph Ludovick umekamilika.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mulungu alisema kwa sasa jalada linaandaliwa kwenda kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa ajili ya hatua zaidi.
Lwakatare na mwenzake, Ludovick, wanakabiliwa na kesi ya ugaidi, katika Mahakama ya Kisutu.
Watu hao wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kufanya mipango ya kumteka na kutaka kumdhuru kwa sumu, Dennis Msacky.
Kuhusu kesi ya kumwagiwa tindikali Kada wa CCM, Mussa Tesha katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa Igunga Septemba 2011, alisema tayari watuhumiwa wawili wamekwishafikishwa mahakamani.
Mulungu alisema kuhusu kuvamiwa, kupigwa na kujeruhiwa kwa Mhariri Mtendaji wa New Habari 2006, Absalom Kibanda, tukio la kutekwa na kujeruhiwa kwa Dk Ulimboka na matukio mengine yaliyotokea Zanzibar, upelelezi bado unaendelea na kwamba upo katika hatua mbalimbali. Aliwataka watu kuwa na subira.