Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kitajitoa
katika mchakato wa Katiba Mpya endapo mambo muhimu mawili hayatapatiwa
ufumbuzi hadi kufikia Aprili 30, mwaka huu.
Wakati Chadema wakisema hayo, Jukwaa la Katiba
Tanzania (Jukata), limesema uchaguzi wa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba
uliomalizika siku tatu zilizopita katika maeneo mbalimbali nchini
haukuwa huru na ni batili, huku likipendekeza urudiwe katika maeneo yote
yaliyokumbwa na kasoro.
Katika hoja zake, Chadema kimesema kinataka
kufutwa kwa uteuzi/uchaguzi wa wajumbe wa Mabaraza ya Wilaya ya Katiba
uliofanywa na Kamati za Maendeleo za Kata na badala yake wajumbe wa
Mabaraza ya Katiba ya Wilaya wachaguliwe moja kwa moja na wananchi wa
Kata husika bila kuchujwa na Kamati za Maendeleo za Kata (WDC).
Msimamo huo ulitolewa na Msemaji Mkuu wa
Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe wakati akisoma hotuba yake ya
makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2013/14 huku akiitaka
Serikali kuwasilisha muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba ili
maeneo kadhaa yafanyiwe marekebisho.