RAIS Paul Kagame wa Rwanda amemteua Mtanzania, Profesa Silas
Rwakabamba kuwa Waziri wa Miundombinu wa nchi hiyo katika mabadiliko ya
Baraza la Mawaziri yaliyofanyika Jumatatu iliyopita.
Kabla ya uteuzi huo, Profesa Rwakabamba
alikuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Rwanda. Ni mmoja wa mawaziri
wanaoingiza sura mpya katika Baraza la Rais Kagame ambalo amelifanyia
mabadiliko kwa kuunda wizara nyingine mpya.
Sura nyingine mpya katika Baraza hilo ambalo
liliapishwa juzi Ikulu ya Rwanda ni pamoja na Seraphine Mukantabana
(Wakimbizi na Menejimenti ya Maafa) na Oda Gasinzigwa (Ofisi ya Waziri
Mkuu- Familia na Jinsia).
Akizungumza kwa simu na mwandishi wetu jana,
mdogo wa Profesa Rwakabamba, Timothy Rwamushaija anayeishi Dar es
Salaam, alisema ndugu yake alizaliwa katika Kijiji cha Bushagara, Wilaya
ya Muleba mkoani Kagera.
Alisema Profesa Rwakabamba alikuwa Mtanzania
aliyeamua kuchukua uraia wa Rwanda na wote baba yao ni Mzee Titus
Rwamushaija... “Huyu ni kaka yangu wa tumbo moja na kwa kweli tumefurahi
sana kwa mafanikio yake sisi kama wanafamilia.”
Naibu Makamu Mkuu - Taaluma wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam(UDSM), Profesa Makenya Maboko alisema Profesa Rwakabamba
alifanya kazi katika chuo hicho na aliondoka akiwa Mkuu wa Kitivo cha
Uhandisi.
“Aliondoka wakati Kagame alipoingia madarakani
na alikwenda kuongoza Taasisi ya Teknolojia ya Kigali (KIST) kabla ya
kwenda katika Chuo Kikuu cha Kigali,” alisema Profesa Maboko.
Msomi huyo alikwenda Rwanda mwaka 1997, baada
ya kuombwa na Rais Kagame ambaye alikwenda UDSM kuwaomba baadhi ya
wahadhiri kwenda Kigali kufungua chuo kikuu katika taifa lake baada ya
kumalizika vita ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1994.
Profesa Rwakabamba alikuwa Mkuu wa kwanza wa
KIST na kukifanya kuwa miongoni mwa vyuo bora barani Afrika kwa masuala
ya teknolojia jambo lililomfurahisha Rais Kagame.
Baada ya mafanikio hayo, Rais Kagame alimteua
kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Rwanda, Butare ambako pia
alijizolea sifa baada ya kusimamia vyema ujenzi wa mabweni kwa wingi na
kiongozi huyo alimtunukia uraia wa nchi hiyo kama zawadi.
Hata hivyo, Profesa Rwakabamba atakuwa
amelazimika kuukana uraia wa Tanzania kwa kuwa katiba ya nchi hairuhusu
uraia wa nchi mbili.
Profesa Rwakabamba alipata elimu ya msingi huko Muleba na akajiunga na Shule ya Sekondari ya Ihungo.
Baada ya hapo, alijiunga na Chuo Kikuu cha
Leeds, Uingereza na kupata Shahada ya Uhandisi mwaka 1971 na 1975
alipata Shahada ya Uzamivu katika fani hiyohiyo.
Chanzo: Mwananchi