Monday, March 27, 2017

WIMBO WA NAY WA MITEGO SASA RUKSA

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Harrison Mwakyembe, ameondoa zuio la kufungiwa kwa wimbo wa ‘Wapo’ wa mwanamuziki Nay wa Mitego.

Akizungumza na waandishi mjini Dodoma leo, Waziri Mwakyembe alimtaka mwanamuziki huyo auboreshe wimbo huo na ikiwezekana aende Dodoma ili akamuongezee maneno zaidi.

Kabla ya kauli ya Dk Mwakyembe ya kuondoa zuio hilo, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) lilizuia kupigwa au kusikilizwa kwa wimbo huo.

 Jana msanii huyo alikamatwa akiwa Morogoro katika shughuli zake za muziki na kuletwa jijini Dar es Salaam, kwa kile kilichoelezwa kuwa wimbo wake umeikashfu serikali.

RIPOTI: FARU JOHN ALIKUFA KWA KUKOSA UANGALIZI WA KARIBU.

Faru maarufu kwa jina John, ambaye alikufa mwaka jana, alikufa akiwa katika hifadhi ya Sasakwa Grumeti kwa kukosa matunzo na uangalizi wa karibu, ripoti ya uchunguzi inasema.

Uchunguzi huo ulioongozwa na Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. Samwel Manyele uligundua kuwa kulikuwa na mapungufu katika kumtunza mnyama huyo kabla ya kufa kwake Prof Manyele amesema miongoni mwa mengine, hakukuwepo na kibali rasmi cha kumhamisha Faru John.
Aidha, hakukuwa na mkataba wa kupokelewa kwa Faru John hifadhi ya Sasakwa Grumeti na afya na maendeleo ya Faru John baada ya kuhamishwa haikufuatiliwa. Prof Manyele alisema hayo alipowasilisha ripoti ya uchunguzi kwa Waziri Mkuu wa Kassim Majaliwa.

"Sababu za kifo chake zilichangiwa na kukosa matunzo na uangalizi wa karibu, kukosa matibabu alipoumwa, mazoea yanayotokana na kutofuata taratibu zilizowekwa kisheria na mapungufu ya kiuongozu kwa Wizara husika, hifadhi na taasisi zake," alisema.

Sunday, March 26, 2017

TANESCO YAIDAI JWTZ BILLION 3.

Mkuu wa Majeshi nchini, Evance Mabeyo amesema Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) linadaiwa Sh3 bilioni na Shirika la Umeme nchini na kesho (Jumatatu)  watapunguza deni hilo ili wasikatiwe umeme.

Mabeyo ameyasema hayo leo wakati anazungumza na waandishi wa habari makao makuu ya jeshi (Ngome) na kueleza deni hilo limetokana na shughuli za jeshi hilo kwenye ulinzi wa Taifa pamoja na ufinyu wa bajeti.

"Baada ya kupokea maelezo ya TANESCO na kufuatia tamko la Rais, Jeshi la Wananchi limetafakari na limefanya jitihada kupata fedha za  kupunguza deni hili, tunadaiwa fedha kiasi kinachozi kidogo Sh3 bilioni, nimeagiza watendaji wetu watafute Sh1 bilioni," amesema Mabeyo.

Mabeyo amesema juhudi zinazofanywa na Jeshi hilo zinatakiwa kuonyeshwa na Taasisi nyingine ili kuweza kuiongezea TANESCO uwezo wa kutoa huduma.

Friday, March 24, 2017

MWIGULU AAGIZA ASKARI ALIEMTISHA NAPE KWA BASTOLA AKAMATWE....!!!

Waziri wa mambo ya ndani Mwigulu Nchemba ameshutumu kitendo cha askari mmoja kuchomoa bastola na kumtisha Nape Nnauye wakati maafisa hao wa usalama walipokuwa wanajaribu kumzuia aliyekuwa waziri wa habari kuhutubia wanahabari.

Mwigulu, kwenye ukurasa wake wa Facebook, amesema kitendo hicho si cha busara na kwamba afisa mhusika kuadhibiwa.

Amesema amemwagiza mkuu wa jeshi la polisi kutumia picha zilizopigwa wakati wa tukio hilo kumska mhusika.

 "Nape Moses Nnauye sio jambazi, ni mtanzania, ni mbunge, mjumbe wa NEC wa CCM, hana record ya uhalifu. Kitendo cha mtu kumtolea bastola, sio cha kiaskari, sio cha kitanzania na sio cha ki Mungu, kama mtu ameweza kutoa bastola mbele ya kamera nawaza mbali ingekuwa kwenye uchochoro angefanya nini," ameandika.

"Nahusika na usalama wa raia wote wa Tanzania, nimemwelekeza IGP atumie picha kumsaka mtu yule aliyeinua kufanya kitu cha kihalifu kwa kofia ya uaskari. Na kama ni askari basi sheria zinazoongoza taasisi husika zichukue mkondo wake.

Sunday, March 19, 2017

ZANZIBAR YAANZA KULIPA DENI LA UMEME

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imeanza kulipa deni lake inalodaiwa na shirika la umeme Tanzania (TANESCO).

Taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa imesema kuwa Profesa Muhongo amesema SMZ imelipa kiasi cha Sh10 bilioni na itaendelea kulipa deni hilo hadi litakapomalizika.

Tuesday, March 14, 2017

WANANCHI WAANDAMANA NA JENEZA HADI KWA DIWANI, WATAKA KUZIKA OFISI KWAKE.

Wananchi wa Kata ya Mhongolo mjini Kahama jana waliandamana wakiwa na  jeneza la mtoto aliyefariki mtaani hapo kwa lengo la kwenda kuuzika mwili huo kwenye Ofisi ya kata hiyo wakidai diwani wa kata hiyo, Michael Mizubo ameuza eneo la makaburi kwa maslahi yake binafsi.

Mmoja wa wananchi hao aliyejulikana kwa jina moja la Paulina ambaye alikuwa akiongoza maandamano hayo, amesema waliamua kwenda kuzika mwili huo wa mtoto huyo aliyejulikana kwa jina moja la Rosemary aliyefariki kwa ugojwa wa kawaida kwenye ofisi hiyo ya kata, kwa sababu hakuna eneo la kuzika.

Hata hivyo wakati wanachimba kaburi hilo kwenye mlango wa ofisi ya diwani huyo kwa lengo la kuuzika mwili huo polisi walifika na kuwatawanya kwenye eneo hilo kwa madai ni ukiukwaji wa taratibu.

Kwa upande wake diwani wa kata hiyo Mizubo anayedaiwa kuuza eneo la maziko amesema  wananchi hao walikuwa na sababu zao za kisiasa kwani pamoja na eneo hilo la makaburi kuuzwa tayari kuna eneo jingine limetengwa kwa ajili ya maziko hayo.

Chanzo: Gazeti la Mwananchi.

TRUMP HAJUI APELEKE WAPI DOLA 400,000 ZA MSHAHARA WAKE

Rais wa Marekani Donald Trump

Msemaji wa ikulu ya White House amesema Rais Donald Trump atatoa mshahara wake kama hisani kwa mashirika yanayosaidia wasiojiweza katika jamii.

Sean Spicer amesema anataka waadhishi wa habari wanaoripoti taarifa kuhusu White House na Rais wa Marekani wamsaidie kuchagua nani wanafaa kupewa pesa hizo.

Mshahara wa Bw Trump utakuwa umefikia dola 400,000 kufikia mwisho wa mwaka.

Wakati wa kampeni za urais, Bw Trump alisema kwamba hakupanga kupokea mshahara wake na kwamba badala yake angepokea dola moja pekee ambayo ni lazima kisheria.

Alikosolewa wakati wa kampeni baada ya taarifa kuibuka kwamba alikuwa ametoa kiwango kidogo sana cha pesa kama hisani licha ya utajiri wake mkubwa.

Saturday, March 11, 2017

SOPHIA SIMBA NA MAKADA WENZIE 11 WATIMULIWA CCM

Chama cha Mapinduzi kimewafukuza makada 12 wa chama hicho wakiwemo wanachama mkongwe kama, Sophia Simba, Ramadhan Madabida na Jesca Msambatavangu.

Wakati wanachama hao wakifukuzwa wengine wanne wamepewa onyo kali,  sita wamevuliwa uongozi na kuwekwa chini ya uangalizi mkali wa miezi 30, huku mwenyekiti wa chama hicho Dodoma, Adam Kimbisa akisamehewa.

 Uamuzi huo umetolewa baada  wa kikao cha Nec kilichofanyika Dodoma leo (Jumamosi) na kuongozwa na mwenyekiti wake, Rais John Magufuli.


 Wengine waliovuliwa uanachama ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni Madenge, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Assa Simba, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara,  Christopher Sanya, Mwenyekiti Mkoa wa Shinyanga Ernest Kwirasa, Mwenyekiti wa Mkoa wa Iringa, Nesta Msabatavunga, Mjumbe wa Halamshauri Kuu (NEC) ya CCM, Ali Sumaye, Mjumbe wa NEC Arumeru, Mathias Manga.

Pia, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Longido Leiza amefukuzwa uanachama pamoja  na Mwenyekiti wa CCM Arusha Mjini, Saileli Molleli, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Gairo, Omary Hawadhi, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Muleba, Mwenyekiti wa CCM Babati, Mwenyekiti wa CCM Wilaya Bunda, Mjumbe wa NEC Gureta.

Waliopewa onyo kali kwa makosa mbalimbali ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Iringa Mjini, Ahmed Kiponza ambaye amepewa onyo kali na kuondolewa madarakani, Mjumbe wa NEC Mkoa wa Singida, Hassa Mzaha, Mwenyekiti wa UWT Gezabulu, Mjumbe wa NEC Kilwa, Ali Mchumo na Mjumbe wa NEC Tunduru, Cheif Kalolo ambaye amevuliwa ujumbe huo na kupewa onyo kali.

WANAOFANYA MAPENZI NA WANAFUNZI KUKAMATWA

Naibu Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo, amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Robert Gabriel, kuwakamata watu wote wanaofanya mapenzi na wanafunzi wa shule za msingi.

Jafo aliyasema hayo juzi wilayani hapa, wakati wa ziara yake ya kutembelea Shule ya Sekondari Mnyuzi na Shule za Msingi za Kilimani na Gereza.

Akiwa kwenye shule hizo, Jafo alikagua na kuridhishwa na thamani ya fedha zilizotumika katika ukarabati wa shule hizo.

Pamoja na hayo, aliwataka viongozi wa wilaya hiyo kutowafumbia macho watu wanaoharibu malengo ya wanafunzi kwa kufanya nao mapenzi.

“Mheshimiwa mkuu wa wilaya, lipo tatizo la wanafunzi wa kike wanaopewa mimba na baadhi ya wanaume.

“Wanaume hao wakamateni, muwaweke ndani kwa sababu hatuwezi kuvumilia vitendo vya aina hiyo kwenye jamii yetu.

“Haiingii akilini kuona wazazi na Serikali wanatumia gharama kubwa kuwasomesha watoto, halafu jitihada hizo zinakwamishwa na waovu fulani, hatuwezi kukubali.

“Sisi kama Serikali, tutahakikisha suala hilo tunalifanyia kazi kwa mapana yake ili liweze kuondoka kwenye jamii kwa sababu tunataka wanafunzi wa kike wasome bila vikwazo,” alisema Jafo.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Robert Gabriel, alimuahidi Jafo kwamba, atafanyia kazi maagizo hayo ili wanafunzi wa kike wasikatishwe masomo yao.

Tuesday, March 07, 2017

YA MH. LISSU KAMA FILAMU VILE

Mambo yanayomtokea kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA) ni kama mchezo wa kuigiza.

Jana, Lissu alianza siku kwa furaha baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu kumuona hana kesi ya kujibu, lakini dakika chache baadaye polisi walimkamata tena, kumhoji na kumuachia kwa dhamana.

Licha ya kashikashi hizo mahakamani na kituo cha polisi, Lissu ameonyesha kuwa na sakata jingine katika uchaguzi wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) baada ya kudai kuwa kuna mkakati unasukwa na baadhi ya mawakili wenzake kutaka kumkwamisha asigombee urais wa chama hicho.

 Baada ya kuachiwa huru, Lissu alikamatwa na polisi akiwa Mahakama ya Kisutu na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi, lakini haikueleweka sababu za kukamatwa kwake.

Lissu alikutana na polisi hao saa 4:00  asubuhi na akaambiwa kuwa anahitajika kituoni, mbunge huyo aliomba aendeshe gari lake mwenyewe ambalo alikuwa nalo Kisutu.
Wakili wake, Fredrick Kihwelo alisema: “Polisi walikubaliana naye na kuingia kwenye gari lake na kuelekea kituoni hapo na walipofika walikaa muda kisha wakaelezwa kuwa, anadaiwa kutoa matamshi yanayoweza kusababisha matatizo ya kidini.”

Alisema Lissu alidaiwa kutoa matamshi hayo akiwa mkoani Dodoma, hivyo baada ya mahojiano aliachiwa kwa dhamana na kutakiwa kuripoti kituoni hapo Machi 13.

Chanzo: Mwananchi.

VIGOGO WA ‘UNGA’ WAHOJIWA

Kazi ya kuchunguza majina 97 yaliyokabidhiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa Kamishna wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, imeanza kufanyiwa kazi kwa vigogo watano waliotajwa kuhojiwa.

Februari 13, Makonda alimkabidhi Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo, Rogers Sianga orodha ya majina 97 ikiwa ni awamu ya tatu ya watuhumiwa wa biashara ya dawa za kulevya.

Kamishna wa Intelijensia wa Mamlaka hiyo, Fredrick Kibula alisema jana kuwa wanawahoji na wanafanya uchunguzi dhidi ya watuhumiwa hao kabla ya kuwafikisha mahakamani.

“Tuna watu muhimu watano wanaotoka katika orodha ile ya mkuu wa mkoa. Tunao kwa ajili ya uchunguzi zaidi na muda ukifika tutawatajia mtawafahamu,” alisema Kamishna Kibula na kuongeza:

“Hatukamati ovyoovyo ni lazima tujiridhishe bila shaka kwamba wahusika wana sifa ya kukamatwa. Pia hatutangazi ingawa tunafanya operesheni za kiuchunguzi ambazo zinafanyika mara kwa mara.”

MAGUFULI AAGIZA TANESCO KUWAKATIA UMEME WASIOLIPA BILI

Rais wa Tanzania John Magufuli jana aliiagiza kampuni ya ugavi wa umeme nchini humo (TANESCO) kuwakatia umeme wateja wote wenye madeni makubwa kwa kampuni hiyo, ikiwemo serikali ya Zanzibar.

Akizungumza kabla ya kuweka jiwe la msingi kwenye kituo kipya cha TANESCO mkoani Mtwara, rais Magufuli alisema kuwa tasisi zote za umma zinapaswa kulipa madeni la sivyo zitakatiwa umeme.

Alisema kuwa serikali ya Zanzibar pekee, kupitia shirika la umeme za Zanzibar (ZECO), ina deni la TANESCO kiasi cha shilingi bilioni 121 za Tanzania.

"Msiogope mnapaswa kukata huduma hii kwa taasisi yoyote ambayo hailipi bili zake. Nataka kumwambia waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo kwamba umeme unapaswa kukatwa hata Ikulu. Nikilala gizani, halafu maafisa wa Ikulu ambao hawajalipa watawajibika na sio wewe. Una hakikisho langu kwa hili.

Saturday, March 04, 2017

NYUMBA YA GWAJIMA YAPIGWA PICHA

Wakili  Peter Kibatala amesema polisi wamepiga picha nyumbani kwa Askofu wa Kanisa la Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima.

Kibatala ambaye ni wakili wa Askofu Gwajima amesema jana kuwa mbali na kupekuwa na kupiga picha kila kona walikwenda katika kanisa lake lililopo Ubungo.

“Waache wafanye yao na sisi tutafanya yetu kisheria. Kwani hatuwezi kuwazuia Polisi kufanya shughuli yao na baada ya kumaliza na sisi tutajua nini cha kufanya,” amesema Kibatala.

Msemaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, David Mngongolwa amesema Gwajima alikwenda jana kuripoti kama alivyoamriwa kufanya hivyo.

Mngongolwa amesema baada ya kuripoti askari walimchukua na kwenda naye nyumbani kwake wakakaa kwa dakika zisizozidi sita na kuondoka naye.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Suzan Kaganda amesema hana taarifa za kukamatwa kwa Gwajima kwa maelezo kuwa alikuwa katika kikao.

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...